Aug 17, 2022 02:35 UTC
  • Russia yaonya kuhusu hatari ya kutokea vita vya moja kwa moja kati yake na Marekani

Ubalozi wa Russia nchini Marekani umeonya kuwa makabiliano baina ya madola hayo mawili makubwa yanaweza kuwa na matokeo yasiyotabirika.

Katika taarifa, ubalozi wa Russia mjini Washington umeonya kuwa tabia ya Marekani katika uga wa kimataifa inaweza kuibua vita vya moja kwa moja baina ya madola hayo mawili yenye silaha za nyuklia.

“Leo Marekani inaendelea kuwa na tabia ya kupuuza usalama na maslahi ya nchi zingine jambo ambalo linaibua hatari ya makabiliano ya kinyuklia,” imesema taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Marekani imechukua hatua ya kukabiliana na Russia kupitia mgogoro wa Ukraine na hali hiyo inaweza kueneza taharuki kwa njia isiyotabirika na kupelekea makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi baina ya madola yenye uwezo wa kinyuklia.”

Ubalozi wa Russia mjini Washington umeitaka Marekani kutathmini sera zake za nyuklia badala ya kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya nchi zingine ambazo sera zao za kimataifa zinakinzana na za Marekani. Aidha taarifa hiyo imesema Russia inatekeleza majukumu yake kama nchi yenye silaha za nyuklia na inachukua kila hatua kuzuia makabiliano ya kinyuklia.

Rais Putin wa Russia

Hayo yanajiri huku mgogoro wa Ukraine uliochochewa na Marekani ukiwa unaendelea bila matumiani ya kufika ukingoni.

Ukraine imekuwa chini ya operesheni ya Russia tangu Februari 24 ambapo Moscow inasema operesheni hiyo inalenga "kuondoa hali ya kijeshi" eneo la mashariki mwa Ukraine la Donbas.

Huko nyuma mwaka wa 2014, mikoa ya Donetsk na jirani yake Luhansk-ambazo kwa pamoja zinaunda Donbas-zilijitangaza kuwa jamhuri huru, zikikataa kutambua serikali ya Ukraine inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi wa NATO. Russia imetambua uhuru wa mikoa hiyo miwili.

Akiamuru kutekelezwa operesheni hiyo nchini Ukraine, Rais wa Russia Vladimir Putin alisema oparesheni hiyo inalenga "kutetea watu ambao kwa miaka minane walikuwa wakiteswa na kutendewa mauaji ya halaiki na serikali ya Kiev."

Mwezi Juni, Putin alionya kwamba nchi yake inaweza kuanza kupanua wigo wa mashambulizi yake nchini Ukraine ikiwa Magharibi itaimarisha usambazaji wake wa silaha kwa nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa sehemu ya Shirikisho la Sovieti.