Aug 17, 2022 07:16 UTC
  • Russia: Uingiliaji wa Marekani katika vita vya Ukraine unazidisha machafuko Asia na Afrika

Mkuu wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Russia amesema kuwa, uingiliaji wa Marekani na waitifaki wake katika vita vya Ukraine umezidisha ukosefu wa utulivu katika eneo la Asia Magharibi na barani Afrika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, Igor Kostyukov amesema hayo katika mkutano wa kimataifa wa usalama uliofanyika mjini Moscow na kutoa ufafanuzi akisema, hatua za Marekani za kujiingiza kwenye vita vya Ukraine zimekuwa na taathira mbaya katika hali ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini bali hata katika maeneo ya nje ya sehemu hizo.

Amesema, dola bilioni 8.5 za misaada ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine na kupeleka nchini humo silaha zisizo na idadi, kumezusha uwezekano wa kuingia silaha hizo mikononi mwa magaidi na hilo ni kwa madhara ya dunia nzima.

Amesisitiza kuwa, tangu vilipoanza vita vya Ukraine, nchi za Magharibi hasa Marekani zimemimina idadi kubwa ya silaha huko Ukraine. Baadhi ya silaha hizo zimeibiwa na zinauzwa kimagendo na bila ya shaka yoyote zinaingia mikononi mwa magenge ya kigaidi.

Igor Kostyukov

 

Hivi karibuni pia televisheni ya Russia Today ilitangaza ripoti inayoonesha jinsi silaha nyepesi na nzito za Magharibi ilizopewa Ukraine, zinavyopigwa mnada na kuuzwa kimagendo. Kwa mujibu wa televisheni hiyo, silaha hizo zinauzwa kwa bei ya kutupa na zinanunuliwa haraka sana. 

Tarehe 24 Februari, Rais Vladimir Putin wa Russia alitoa amri ya kuishambulia kijeshi Ukraine kuitikia ombi la viongozi wa maeneo mawili ya Donetsk na Luhansk ya mashariki ya nchi hiyo, lakini akatangaza kuwa lengo la Moscow ni kuipokonya silaha tu Ukraine na si kuikalia ardhi ya nchi hiyo.

Tags