Aug 18, 2022 02:44 UTC
  • Tamko la Putin kuhusu utayari wa Russia wa kuwapatia waitifaki wake silaha za kisasa kabisa

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, Moscow iko tayari kuwapatia waitifaki wake wa Amerika ya Latini, Asia na Afrika aina mbalimbali za silaha za kisasa kabisa.

Putin ameeleza hayo alipohutubia hafla ya teknolojia za kijeshi za vikosi vya ulinzi vya Russia 2022.

Amefafanua kwa kusema: Russia inapendelea kustawisha katika pande zote mashirikiano ya kijeshi na kiufundi, ambayo ndicho kitu chenye umuhimu katika mpango wa kuwepo dunia ya madola kadhaa yenye nguvu. Moscow inathamini uhusiano wake na nchi za Amerika ya Latini, Asia na Afrika na iko tayari kuzipatia aina mbalimbali za silaha za kisasa kabisa.

Rais Vladimir Putin wa Russia (aliyevaa koti refu jeusi)

 

Rais wa Russia ameendelea kueleza kwamba, "Tuko tayari kuwapatia waitifaki wetu aina za kisasa kabisa za silaha, kuanzia silaha ndogondogo mpaka magari ya deraya, mizinga, ndege za kivita na ndege zisizo na rubani."

Tamko la Putin la kuwa tayari kuziuzia silaha za kisasa nchi waitifaki wa Russia ulimwenguni kote ni ishara ya mageuzi makubwa katika sera za jadi za Moscow katika uuzaji silaha. Kabla ya hapo, Russia ilikuwa ikijiwekea mipaka maalumu katika kuzipatia nchi zingine silaha; na kwa kutoa mfano, Moscow ilikuwa haikubali kuziuzia nchi nyingine silaha zake za kisasa zaidi kama makombora yenye kasi kubwa zaidi kuliko ya sauti. Makombora hayo, kama ilivyoonekana pia katika vita vya Ukraine, yanahesabiwa kuwa ni silaha inayoweza kubadilisha hatima ya vita. Mfano mwngine ni wa mtambo wa ulinzi wa anga na makombora wa S-500, ambao Moscow imeuunda kwa ajili ya vikosi vyake vya ulinzi na hadi sasa haijaiuzia nchi yoyote ile. Ukweli ni kuwa, viongozi waandamizi wa kisiasa na kijeshi wa Russia siku zote wamekuwa na wahka wa kuchelea teknolojia yoyote mpya ya kijeshi ya nchi hiyo isije ikaingia mikononi mwa Magharibi na hasa Marekani; na ndio maana hadi sasa imesita kuzipatia nchi zingine baadhi ya silaha zake za kisasa.

Mtambo wa makombora wa S-500

 

Lakini kutokana na matukio yaliyojiri karibuni, hali na mazingira hivi sasa yamebadilika kikamilifu Kwa upande mmoja kujiri kwa kujiri vita vya Ukraine, Wamagharibi wakiongozwa na Marekani, wamehisi hii ni fursa mwafaka ya kuweka vikwazo vikali zaidi na ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika pande na nyuga zote dhidi ya Russia zikiwemo za kidiplomasia na kisiasa na kuifanya ndio ajenda yao kuu kampeni ya kuitenga zaidi na zaidi Moscow katika uga wa kimataifa. Ni kutokana na suala hilo, ndipo Moscow nayo ikaamua ichukue hatua ya kujibu mapigo kwa kustawisha uhusiano wake na nchi za maeneo mengine ya dunia. Katika hatua ya kwanza, suala hilo limedhihirika katika kustawishwa uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na nishati wa Russia na nchi zingine kama China na India. 

Pamoja na hayo, kwa kutilia maanani kwamba Russia ni nchi ya pili inayouza silaha kwa wingi zaidi duniani, ni wazi kuwa moja ya nukta kuu katika muelekeo mpya ulioonyeshwa na Moscow ni kutangaza sera mpya za uuzaji silaha, ambapo kwa kuzingatia hotuba ya siku ya Jumatatu iliyotolew na Putin hakutakuwa tena na kizuizi au mpaka wowote katika suala hilo. Kwa kuzingatia bei ya chini ya silaha za Russia pamoja na ubora wake kuna uwezekano mkubwa muelekeo huu mpya utazifanya baadhi ya nchi zivutiwe zaidi kununua silaha kutoka Moscow na hivyo kufunga mikataba mipya ya ununuaji silaha kwa nchi hiyo.

Silaha za kivita zinazoundwa nchi za Magharibi

 

Kwa upande mwingine, na kwa kuzingatia kuwa hivi sasa Russia inakabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni kutokana na vikwazo vya Magharibi, nchi hiyo imekuwa na hamu zaidi ya kuuza silaha zake kwa nchi zingine ili kwa njia hiyo, mbali na kuendeleza na kustawisha soko lake la uuzaji silaha iweze pia kujipatia mapato ya fedha za kigeni. Kuhusiana na nukta hiyo, Putin mwenyewe amesema: Moscow iko tayari kustawisha uhusiano na ushirikiano kwa ajili ya kuunda zana mpya za aina mbalimbali na vilevile kushirikiana katika hali na mazingira sawa. Kwa kustawisha mashirikiano mapana ya kijeshi na kiufundi  itawezekana kuzihakikishia usalama wa kuaminika nchi zenye uhusiano na ushirikiano duniani. Suala jengine kuhusiana na nukta hiyo, kwa kutilia maanani jitihada za mtawalia zinazofanywa na Russia za kuanzisha dunia ya kambi kadhaa zenye nguvu, ni kupungua utegemezi wa nchi za dunia kwa silaha za Magharibi, ambao umeandaa mazingira ya madola hayo na hasa Marekani ya kuzitwisha nchi wanunuzi matakwa yao, hali inayozidi kuimarisha ubeberu na nguvu za Magharibi za kuhodhi na kutawala siasa za dunia.

Bila shaka kubadilisha Russia muelekeo wake wa uuzaji silaha hautayafurahisha madola ya Magharibi na hasa Marekani, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imefanya jitihada kubwa kwa kutumia sheria yake ya vikwazo ya CAATSA kuzizuia nchi zingine zisinunue silaha kutoka Russia, ambapo kwa kutumia vitisho na mbinu ya kurubuni imeweza hata kuvurga baadhi ya mikataba ya mauzo ya silaha kati ya Russia na nchi kama Misri na Indonesia.../

Tags