Aug 19, 2022 04:04 UTC
  • China: Uhuru wa Taiwan maana yake ni vita

Balozi wa China mjini London ameonya kuwa, uingiliaji wa mambo unaofanywa na Uingereza na Marekani juu ya suala la Taiwan hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya vita.

Zheng Zeguang, Balozi wa China nchini Uigereza ametoa indhari hiyo katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la The Guardian na kueleza kuwa, kwa miaka mingi sasa, Marekani imekuwa ikitumia suala la Taiwan kujaribu kuidhibiti China, na kuimarisha mauzo ya silaha zake kwa kisiwa hicho. 

Mwanadiplomasia huyo amesema: China inaiasa Marekani iache kucheza karata ya Taiwan na isishadidishe zaidi mgogoro. Hakuna sababu yoyote kwa Uingereza kupuuza ukweli huu na kufuata nyayo za Marekani.

Siku chache zilizopita, Taipei ilidai kuwa China inapanga njama ya kukivamia kisiwa cha Taiwan, baada ya Beijing kutangaza duru mpya ya mazoezi ya kijeshi katika maji ya kisiwa hicho, ukiwa ni muendelezo wa kujibu mapigo kwa ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi katika kisiwa hicho hivi karibuni.

Luteka ya China pambizoni mwa Taiwan

Beijing inasisitiza kuwa, hatua ilizochukua ni jibu kwa kitendo cha Pelosi cha kuitembelea Taiwan mapema mwezi huu, na kwamba ziara hiyo ilikuwa uingiliaji wa masuala ya ndani ya Jamhuri ya Watu wa China mbali na kukiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Asia.

Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China, na imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan; na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.

Tags