Aug 19, 2022 04:04 UTC
  • UN: Utumwa mamboleo umekita mizizi kote duniani

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusiana na kuongezeka maafa ya utumwa mamboleo katika maeneo mbalimbali duniani.

Katika ripoti yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tomoya Obokata amesema janga la utumwa mamboleo limekita mizizi kote duniani, hususan kutumikishwa watoto wadogo.

Obokata ameeleza kuwa, "Katika maeneo ya Asia, Pacific, Mashariki ya Kati, Amerika na Ulaya, asilimia 4 hadi 6 ya watoto wanatumikishwa."

Ripota maalumu wa UN amesema kuwa, asilimia 21.6 ya watoto barani Afrika wanakabiliwa na utumwa mamboleo, huku asilimia 23.9 ya watoto katika eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika wakitumikishwa na kupewa kazi za sulubu.

Nchi za Afrika zinazoongoza kwa utumwa mamboleo ni Mauritania, Mali na Niger katika eneo la Sahel barani humo, huku baadhi ya wanawake wakiwa watumwa na hususan watumwa wa ngono kwa magenge ya kigaidi kama Boko Haram.

Kutumikishwa watoto katika matimbo ya madini barani Afrika

Afisa huyo wa UN amebainisha kuwa, sababu ya ongezeko la idadi ya watumwa mamboleo ni mabadiliko ya tabianchi, uhajiri na mabadiliko ya kijiografia ya wanadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya milioni 40 kote duniani wanasumbuliwa na utumwa mamboleo. Nayo ripoti ya shirika la kupambana na utumwa la Walk Free Foundation lenye makao makuu yake nchini Australia inasema kuwa, mamilioni ya watu wanaandamwa na utumwa kote duniani hii leo, na kwamba ni muhali kutokomeza utumwa kufikia mwaka 2030 kama ilivyopasishwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa miaka 7 iliyopita.

Tags