Aug 19, 2022 09:17 UTC
  • Kuuawa Mawlawi Mehdi Mujahid, kamanda wa zamani wa Taliban kwa kulipinga kundi hilo

Wizara ya Ulinzi ya Taliban nchini Afghanistan imetangaza habari ya kuuawa Mawlawi Mehdi Mujahid, kamanda wa zamani wa kundi hilo kutoka kabila la Hazara na ambaye alikuwa haridhishwi na utendaji wa kundi hilo. Kamanda huyo ameuawa kwa kupigwa risasi na Taliban huko Herat, magharibi mwa Afghanistan.

Muhammad Mohaqiq, Mkuu wa Chama cha Umoja wa Kiislamu cha Wananchi wa Afghanistan amelaani vikali mauaji hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook na kuandika, askari wa kundi la Taliban walimuwekea mtego Mawlawi Mehdi Mujahid katika kijiji cha Bunyad huko Herat na baadaye kumtia mbaroni.

Muhammad Mohaqiq  pia ameandika, kwa mujibu wa madai ya wizara ya ulinzi ya Taliban, Mawlawi Mehdi Mujahid alipigwa risasi na kuuliwa na kundi hilo baada ya kutolewa hukumu dhidi yake katika mahakama moja ya jangwani. 

Kuuliwa Mehdi Mujahid ambaye aliamua kujitoa kwenye kundi la Taliban kwa kutoridhishwa na utendaji wake, unaweza kuwa ndio mwisho wa mapigano ya miezi miwili katika eneo la Balkhab huko Afghanistan.

 Mawlawi Mehdi Mujahid

 

Mapigano baina ya wapiganaji wa kundi la Taliban na wale wa Mawlawi Mehdi Mujahid ambaye kabla ya kujitenga na Taliban alikuwa mkuu wa idara ya kijasusi ya kundi hilo katika wilaya hiyo ya Balkhab mkoani Sar-e Pol, yalianza baada ya Mehdi Mujahid kulishutumu kundi la Taliban kuwa ni la kikabila na linafanya ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya watu wa kaumu na makabila mengine nchini Afghanistan.

Miezi miwili iliyopita, kundi la Taliban lilipeleka mamia ya wapiganaji wake katika wilaya ya Balkhab, wakaanza kufanya msako wa nyumba kwa nyumba, wakazusha kwa makusudi hali ya hofu na woga mkubwa kati ya wakazi wa wilaya hiyo na kumkandamiza kila aliyetiliwa shaka kuwa anamuunga mkono Mawlawi Mehdi Mujahid kwa namna yoyote ile.

Utaratibu uliotumiwa na serikali ya Taliban wa kumuua Mawlawi Mehdi Mujahid unaonesha kuwa kundi hilo linaamini kwamba, kwa kumuua kamanda wake huyo wa zamani aliyejitenga na kundi hilo, kutaweza kunyamazisha kilio cha wakazi wa mkoa wa Sar-e Pol wanaolalamikia siasa za kibaguzi za Taliban. Kundi hilo limeonya kuhusu hatua yoyote ya kuanzisha upinzaji wa silaha dhidi ya serikai yake. 

Wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan

 

Watu wengi Afghanistan walitaraji kuwa kundi la Taliban lisingelikabiliana kwa nguvu za silaha na Mawlawi Mehdi Mujahid, bali lingesikiliza kilio cha wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine ya Afghanistan na kuzivutia nyoyo za wananchi wote wa nchi hiyo kwa siasa sahihi na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa baina yao.

Muhammad Mohaqiq, ni miongoni mwa wanasisa wakubwa wa serikali iliyopita na ni mkuu wa Chama cha Umoja wa Kiislamu cha Wananchi wa Afghanistan. Anasema hivi kuhusu hatua ya Taliban ya kutumia nguvu za silaha huko Balkhab na kumuua kwa risasi Mawlawi Mehdi Mujahid: Jambo la busara na la kimantiki lilikuwa ni Taliban kutatua kwa njia ya mazungumzo matatizo yake na kamanda wake huyo ambaye ndiye pekee aliyejiunga na kundi hilo kutoka kwa watu wa kabila la Hazara. Lakini hatua ya Taliban ya kupeleka mamia ya wapiganaji wake katika wilaya ya Balkhab kwenda kumkandamiza kamanda wake huyo, bila ya shaka kutahesabiwa kuwa ni kutangaza vita na watu wote wa kabila la Hazara na hilo si kwa manufaa ya mtu yeyote yule.

Mapigano ya miezi miwili yaliyotokea baina ya wapiganaji wa kundi la Taliban na wale wa kamanda wake wa zamani, Mawlawi Mehdi Mujahid huko Balkhab na ambayo yamepelekea kuuawa na kujeruhiwa wapiganaji wengi wa pande zote mbili na pia kukosa makazi mamia ya watu katika eneo hilo, yamezidisha hali ya wasiwasi ndani ya Afghanistan huku Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yakitoa onyo kali kuhusu madhara ya mizozo hiyo ya kutumia silaha. Aidha mapigano hayo yamezidi kuipa kisingizio jamii ya kimataifa cha kutokuwa na imani na serikali ya kundi la Taliban. Maana ya jambo hilo ni kuendelea mateso kwa wananchi wa Afghanistan ambao hata hivi hivi sasa wako chini ya vikwazo, mashinikizo na hali mbaya ya maisha kutokana na serikali ya kundi la Taliban kususiwa na jamii ya kimataifa.

Tags