Aug 19, 2022 10:57 UTC
  • WHO: Corona haijamalizika, nchi zichukue hatua madhubuti kukabiliana nayo

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuhusiana na msambao wa kirusi cha corona kuwa, usambaaji wa kirusi hicho haujamalizika na kwamba nchi duniani zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana nacho.

Kirusi cha corona kiligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini China Desemba 2019. Hadi sasa zaidi ya watu 599,124,439 wameambukizwa kirusi hicho duniani kote na zaidi ya 6,466,793 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi hicho. Jumla ya watu 573,112,063 wameugua ugonjwa huo lakini wamepata nafuu.

Katika ripoti yake, WHO imesema, hadi kufikia wiki iliyopita, maambukizi mapya ya corona duniani kote yalipungua kwa kiwango cha theluthi moja na idadi ya vifo ilipungua kwa asilimia sita, lakini idadi ya walioambukizwa katika baadhi ya maeneo ya bara la Asia imeongezeka.

Shirika la Afya Duniani limebainisha pia kwamba, takwimu mpya za wiki iliyopita zinaonyesha kuwa, watu milioni tano na laki nne wamepata ugonjwa wa Covid-19, ambapo kulinganisha na wiki mbili zilizopita wamepungua kwa asilimia 24.

 

Katika mabara ya Afrika na Ulaya pamoja na eneo la Magharibi ya Asia, maambukizi ya kirusi cha corona yamepungua kwa asilimia 40, lakini katika baadhi ya sehemu za mashariki ya Asia na eneo la Magharibi ya Oceania, idadi ya vifo imeongezeka kwa asilimia 31.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom amesema, katika mwezi uliopita idadi ya vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona iliongezeka kwa asilimia 35, ambapo wiki iliyopita viliripotiwa vifo vya wagonjwa elfu 15.

Adhanom ameongeza kuwa, kirusi cha corona kinasambaa kwa uhuru lakini nchi duniani hazichukui hatua madhubuti na athirifu kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi hicho…/

 

Tags