Aug 19, 2022 12:19 UTC
  • Mexico: Kutoweka wanachuo 43 mwaka 2014 ulikuwa “uhalifu wa kiserikali”

Viongozi wa serikali ya Mexico wamesema, kutoweka wanachuo 43 mwaka 2014 ambako kulififilishwa na serikali ya wakati huo ilikuwa “jinai na uhalifu wa kiserikali.”

Septemba 26, 2014 wanafunzi 43 wa vyuo vikuu walitoweka katika mji wa Iguala katika kile kilichotajwa kuwa ni utekajinyara wa halaiki. Tukio hilo lilijiri kufuatia ukandamizaji uliofanywa na polisi wa eneo hilo baada ya wanachuo hao kushiriki maandamano ya upinzani yaliyofanyika katika mji mkuu Mexico City.

Rais Andrés Manuel López Obrador wa Mexico ametupilia mbali ripoti za serikali iliyopita ya wakati huo na kuahidi kuwa atafichua na kuweka hadharani kila kilichojiri kuhusiana na wanachuo hao katika tukio la Septemba 2014 katika mji wa Iguala kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Kutoweka wanachuo hao 43 nchini Mexico na kutochukuliwa hatua yoyote wahusika kulilaaniwa kimataifa na kuchafua taswira ya serikali ya rais wa wakati huo Enrique Peña Nieto, hasa baada ya wataalamu wa kimataifa wa haki za binadamu kukosoa uchunguzi uliojaa kasoro na utumiaji mbaya wa mamlaka uliofanywa na maafisa wa serikali hiyo.

Jamaa wa familia za wanachuo walipoandamana kutaka ifahamike hatima ya wanafunzi hao

 

Katika hatua isiyo ya kawaida, afisa mmoja mwandamizi wa masuala ya haki za binadamu wa serikali ya Mexico alitangaza rasmi kuwa, hakuna dalili yoyote inayoonyesha kuwa wanachuo hao wangali hai.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi iliyotolewa mwaka 2015 na rais wa wakati huo Enrique Peña Nieto, genge moja linalojihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, liliwakamata kimakosa wanafunzi hao kwa kuwafananisha na wanachama wa genge hasimu, wakawaua na kisha wakazichoma moto maiti zao jalalani…/