Aug 21, 2022 08:20 UTC
  • Kuanzisha uchunguzi Polisi ya Ujerumani dhidi ya Rais wa Palestina kuhusiana na Holocaust; undumakuwili mwingine wa Magharibi

Polisi ya Ujerumani imesema, imeanzisha uchunguzi dhidi ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa sababu ya kauli aliyotoa kuhusu Holocaust, yaani mauaji ya halaiki ya Wayahudi yanayodaiwa kufanywa na utawala wa Kinazi wa Ujerumani chini ya uongozi wa Adolf Hitler.

Katika taarifa iliyotoa siku ya Ijumaa ya Agosti 19, Polisi ya Berlin ilisema, uchunguzi huo uko kwenye hatua za awali na kwamba baada ya kupokea malalamiko rasmi ya kisheria, tayari imeshachukua hatua zinazohitajika kuhusiana na suala hilo.

Mahmoud Abbas, ambaye alikuwa ziarani nchini Ujerumani kwa mwaliko rasmi wa Kansela Olaf Scholz wa nchi hiyo, siku ya Jumanne ya tarehe 16 Agosti alifanya mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake huyo, ambapo aliulizwa na mwandishi mmoja wa habari: "una nia ya kuomba radhi kwa shambulio la kigaidi lililofanywa na vikosi vya Wapalestina katika michezo ya Olimpiki miaka 50 iliyopita na kupelekea kuuawa wanamichezo wa Israel?" Na yeye akajibu kwa kusema: "kama mnataka kuangalia yaliyotokea nyuma, fanyeni hivyo; kwani kuanzia mwaka 1947 hadi sasa, Israel imeshafanya mauaji 50 ya Holocaust katika sehemu 50 za Palestina".

Mahmoud Abbas (kushoto) na Olaf Scholz katika mkutano na waandishi wa habari

 

Kauli hiyo ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina iliukasirisha utawala wa Kizayuni wa Israel; na Tel Aviv ikazitaka nchi duniani zitoe msimamo juu ya suala hilo. Katika mkutano huo na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Abbas, Kansela wa Ujerumani hakuonyesha msimamo wowote, lakini katika taarifa rasmi aliyotoa baadaye kwa vyombo vya habari alisema, matamshi aliyotoa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuifanya Holocaust ionekane si jambo lenye umuhimu mkubwa, yanachukiza.

Hisia zilizoonyeshwa na serikali ya Ujerumani na kuanzisha uchunguzi Polisi ya nchi hiyo kuhusu matamshi aliyotoa Mahmoud Abbas kuhusiana na Holocaust kwa kusisitiza kwamba utawala wa Kizayuni umeshafanya mara kadha wa kadha Holocaust dhidi ya Wapalestina, vinadhihirisha vipimo vya undumakuwili vinavyotumiwa na Wamagharibi katika suala la uhuru wa kutoa maoni. Kwa mtazamo wa Wamagharibi kuyatusi na kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, kama kuchapisha vikatuni vya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW bila kujali na kuzingatia matukufu ya Waislamu ni kielelezo cha uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, lakini kuhoji au kutilia shaka tu Holocaust na kuyafananisha na mauaji ya kimbari ya kila leo yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina huwa ni kosa lisilosameheka.

Kansela wa Ujerumani amelaumiwa kwa kuchelewa kuchukua hatua dhidi ya matamshi ya Rais wa Palestina

 

Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hasa Ujerumani, ambazo ni waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel, zimekuwa zikiupatia kila leo utawala huo misaada mingi, tena si ya kifedha, kiuchumi, silaha na ya kinyuklia pekee, bali hata katika upande wa kiutamaduni na kihistoria pia zimeonyesha mara kadhaa uungaji mkono wao kwa Israel. Katika baadhi ya nchi za Ulaya zimepitishwa sheria maalum za kupiga marufuku kutilia shaka mauaji ya Holocaust, ambapo mtu yeyote anayejusuru kuhoji au kutilia shaka ukubwa wa maafa ya Holocaust, kuhusu namna yalivyotokea au kutaka kufanya uchunguzi juu ya kadhia hiyo, huchukuliwa hatua za kisheria kwa kushtakiwa na kuishia kutozwa faini au kuhukumiwa kifungo jela.

Katika nchi kadhaa kama Ujerumani, Austria, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, Lithuania, Poland, Romania, Slovakia na Uswisi zimetungwa sheria dhidi ya wakanushaji wa Holocaust. Na ndio maana hadi sasa kuna shakhsia kadhaa wa kiakademia na kisiasa ambao wameadhibiwa kwa sababu ya kutilia shaka tu ukweli kuhusu ukubwa wa maafa ya Holocaust. Mmoja wa watu hao ni David Irving, mwandishi na mwanahistoria wa Uingereza ambaye mwaka 2006 alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kuyakana mauaji hayo. Roger Garaudy, mwanafaslafa na mwandishi wa Ufaransa, ambaye alifariki dunia mwaka 2012, naye pia alitiwa hatiani na kutozwa faini kwa kukanusha mauaji ya Holocaust. Mwalimu na mwandishi wa Uswisi Jürgen Graf, naye pia mwaka 2000 alihukumiwa kifungo jela kwa kukanusha Holocaust; na ili kuepuka kifungo, ilimlazimu kuihama nchi yake yeye na familia yake; na tangu wakati huo hadi sasa anaishi uhamishoni nchini Russia.

Mwanahistoria David Iriving

 

Pamoja na kwamba Wamagharibi wenyewe ndio wasababishaji wa maafa hayo ya kibinadamu yaliyopewa jina la Holocaust, lakini si tu wamekitumia kisingizio hicho kuunga mkono uwepo wa utawala bandia wa Kziayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina kwa gharama ya kuwageuza wakimbizi mamilioni ya wananchi wa ardhi hiyo, lakini hivi sasa pia na baada ya kupita karibu miaka 77 tangu yalipotokea maafa hayo ya Holocaust wanaendelea kuwalipa fidia waathirika wake; na wale wanaohoji au kutilia shaka ukubwa wa maafa ya tukio hilo au mtu kama Mahmoud Abbas aliyejaribu tu kufananisha Holocaust na mauaji ya kinyama ya Wapalestina yanayofanywa kila leo na Wazayuni, wanaandamwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.../

  

Tags