Sep 10, 2022 08:13 UTC
  • FBI katika hali ya tahadhari baada ya kuvamia nyumba ya Trump

Maafisa wa usalama wa Marekani wamewekwa katika hali ya tahadhari baada ya Polisi ya Upelelezi ya Shirikisho la Marekani (FBI) kuvamia makazi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump.

Mnamo Agosti 8, maafisa wa FBI walivamia jumba la kifahari la Donald Trump huko Florida linalojulikana kama "Mar-e-Lago" na kukamata masanduku 33 ya hati, pamoja na seti 11 za nyaraka za siri, kutoka kwenye makazi yake. Kulingana na ripoti ya New York Times, Trump alichukua nyaraka zisizopungua 300 za siri kwenye jumba lake la kifahari.

Mtandao wa habari wa Bloomberg umeandika katika ripoti yake kuwa rekodi zinaonesha kuwa maafisa wakuu wa FBI walikuwa katika hali ya tahadhari muda mfupi baada ya uvamizi wa makazi ya rais wa zamani, Donald Trump, wakihofia uwezekano wa kutokea ghasia nchini Marekani.

Katika sehemu nyingine ya ripoti yake Bloomberg imesema maafisa wa ujasusi, ambao wana jukumu la kulinda vituo na majengo ya serikali, wametoa wito wa kuongezwa kwa doria na usalama karibu na milki na taasisi za serikali na kuamuru maafisa watendaji kuwa katika utayarifu kamili.

Wakati huohuo tovuti ya habari ya Politico imeripoti kuwa Polisi ya Upelelezi ya Marekani inafanya uchunguzi dhidi ya Trump kwa sababu ya kuteketeza nyaraka, kuweka vizuizi vya kukwamisha uchunguzi na kukiuka sheria ya ujasusi ya nchi hiyo.

Mapema mwaka huu Idara ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Marekani ilitangaza kuwa, nyaraka za taarifa za siri zimepatikana kwenye maboksi 15 ya kumbukumbu za Ikulu ya White yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump huko Mar-a-Lago, jimboni Florida.

Hayo ni kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Idara hiyo ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa kwa Wizara ya Sheria.

Barua hiyo imetolewa kufuatia ripoti kadhaa kwamba Trump amekuwa akihodhi taarifa hasasi, nyeti na hata za siri za serikali tangu wakati wa kipindi chake cha urais na hata baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Sheria ya serikali kuu ya Marekani inapiga marufuku kuzihamishia sehemu isiyoruhusika nyaraka za siri za serikali.

Tags