Sep 12, 2022 08:21 UTC
  • Kupenda vita Marekani duniani; urithi wa tukio la Septemba 11

Jumapili ya jana tarehe 11 Septemba ilisadifiana na kutimia miaka 21 tangu kutokea mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 ambapo hadi sasa Marekani ingali imeshughulishwa na matokeo ya tukio hili lenye kuainisha hatima.

Tukio la Septemba 11 linaweza kutajwa kuwa, sababu halisi ya kuanza duru na zama mpya katika uhusiano wa kimataifa. Mashambulio ya Septemba 11, 2001 yalipelekea kutokea mienendo na matukio katika uga wa kimataifa na kieneo hususan Asia Magharibi ambayo licha ya kupita zaidi ya miongo miwili tangu kutokea kwake, lakini athari zake zingali zimebakia. Hili linaweza kuwa nukta ya kianzio katika sera za kigeni za Marekani.

Baada ya tukio la Septemba 11, Rais wa wakati huo wa Marekani George W. Bush alitoa amri ya kushambuliwa Afghanistan na Iraq kwa kile kilichotajwa kuwa, vita dhidi ya ugaidi. Katika vita hivyo vilivyojulikana kama eti vita vya kimataifa dhidi ya ugaidi, zaidi ya watu milioni waliuawa bure bilashi katika mataifa ya Iraq, Afghanistan, Syria, Libya na Yemen.

Kukaliwa kwa mabavu Iraq na matokeo yake mabaya ya hatua hiyo, hatimaye kulipelekea kuibuka makundi ya kigaidi kama Daesh ambalo limefanya mauaji mengi na ya kutisha katika nchi za Iraq na Syria. Pamoja na hayo, Marekani haikupata natija yoyote kwa hatua yake ya kutuma majeshi katika nchi hizo ambapo mwaka jana (2021) ililazimika kuondoka Afghnaistan ikiwa imeinamisha kichwa chini baada ya kushindwa kufikia malengo yake. Pamoja na hayo, Marekani ingali ina uwepo wa kijeshi huko Iraq na Syria.

Shambulio la Septemba 11

 

Vita hivyo, mbali na kusababisha mauaji na kujeruhiwa maelfu ya wanajeshi wa Marekani, vimekuwa na gharama kubwa mno kwa bajeti ya dola hilo la kibeberu linalopenda vita. Rais aliyetangulia wa Marekani Donald Trump alidai kwamba, gharama ya vita hivyo imefikia dola trilioni 7. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, baada ya tukio la Septemba 11, washindi halisi wa hatua za kijeshi za Marekani ni mashirika na makampuni ya kuzalisha silaha nchini Marekani.

Taasisi ya Masuala ya Umma na ya Kimataifa  ya Chuo Kikuu cha Brown imesema katika moja ya ripoti zake kwamba, nusu ya majimui ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon katika miaka ya 2000-2020 ambayo inafikia dola trilioni 14 ilikuwa hisa ya makampuni na mashirika ya uzalishaji silaha nchini humo. Aidha dola trioni 4.4 katika fedha hizo zilikuwa hisa ya viwanda vya kijeshi vya Marekani.

Charles Strozier, mwanahistoria na mchambuzi wa kimataifa anasema: Mashambulio ya Septemba 11 yalileta mgogoro mkubwa wa uwepo wa Marekani ambapo kufuatia hilo, Washington ikaibuka na kuwa kama “mnyama aliyejeruhiwa” na kutumbukia katika kinamasi cha vita na hatimaye kasi yake ya kuporomoka ikaongezeka.

Jambo jingine ambalo liko wazi ni kuwa, tukio la Septemba 11 limekuwa na mchango mkubwa katika kushadidisha chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya Waislamu nchini Marekani. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka 21 iliyopita na baada ya tukio la Septemba 11, mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani umechukua mkondo wa kuongezeka. Akthari ya Waislamu nchini Marekani wanahisi kwamba, wamekuwa wakiandamwa, kubaguliwa, kukandamizwa na hata kuvunjiwa heshima kwa kuhusishwa na makosa ambayo kimsingi hawajayafanya wala hawajayaunga mkono.

Chuki dhidi ya Uislamu zimeshadidi nchini Marekani

 

Chuki dhidi ya Uislamu na hujuma pamoja na mashambulio yanayotokana na chuki dhidi ya Waislamu zilichukua wigo mpana zaidi hususan katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump. Mwanasiasa huyo mbaguzi akitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi alielekeza hujuma zake dhidi ya Waislamu.  Hatua yake ya kutoa agizo la kupiga marufuku kuingia nchini Marekani raia wa nchi 6 za Kiislamu na kuwaita kuwa ni magaidi ni ishara ya wazi ya utendaji wa upande mmoja wa Donald Trump.

Kimsingi tunapaswa kusema kuwa, misimamo na hatua za serikali ya Marekani ni moja ya sababu za kushadidi mtazamo mbaya na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa Marekani hususan katika kipindi cha urais wa Donald Trump.

Mildred Elizabeth Sanders, mhadhiri wa Chuo Kikuu wa Kimarekani anasema kuwa, moja ya mabadiliko makubwa katika jamii ya Marekani baada ya tukio la Septemba 11 ni kujitokeza hali ya woga baina ya Waislamu na kuongezeka mtazamo mbaya dhidi ya Saudi Arabia.

George W. Bush Rais wa zamani wa Marekani

 

Kunapozungumziwa tukio la Septemba 11 hujitokeza jambo moja nalo ni juhudi za Marais wa Marekani kuanzia George W. Bush hadi Donald Trump za kujaribu kufunika nafasi ya Saudia katika kuwaunga mkono waliotekeleza mashambulio hayo kwa kisingizio cha kuwa na taathira hasi hilo katika uhusiano wa Riyadh na Washington.

Baada ya Joe Biden kuingia madarakani licha ya kuwa awali alionyesha kuwa atachukua hatua kali dhidi ya Saudi Arabia na hata kudai kutazama upya uhusiano wa nchi yake na Riyadh, lakini hatimaye aliamua kuendeleza uhusiano uleule wa hapo kabla kutokana na kuzingatia maslahi ya kiuchumi na kistratejia ya nchi yake kwa Saudia; na hivyo kuanza tena kuiuzia silaha nchi hiyo ya Kiarabu.

Licha ya madai ya Marekani ya kupambana na ugaidi katika uga wa kimataifa, lakini kuhusiana na masuala kama uungaji mkono wa Saudia kwa watekelezaji wa shambulio la kigaidi la Septemba 11 ambalo linahesabiwa kuwa ni moja ya matukio makubwa ya kigaidi katika karne ya 21, Washington imeamua kufumbia macho kikamilifu ukweli huo usiokanushika.

Tags