Sep 14, 2022 12:06 UTC
  • Kitabu kipya chafichua hofu ya Trump ya kulipiziwa kisasi na Iran kwa mauaji ya Kamanda Soleimani

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, aliwaambia rafiki zake kabla ya kumalizika muhula wake wa urais kuwa, alikuwa akihofia kwamba Iran ingejaribu kumuuwa ili kulipiza kisasi mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduuzi ya Kiislamu (Sepah). Hayo ni kwa mujibu wa kitabu kipya.

Luteni Jenerali Soleimani aliuliwa shahidi katika shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) ya Marekani kwa amri ya moja kwa moja ya Trump karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad Januari 3, 2020. Abu Mahdi al Muhandes aliyekuwa Naibu Mkuu wa harakati ya wapiganaji wa kujitolea wa Iraq ya al Hashdu Shaabi na wanajihadi wengine 8 pia waliuliwa katika hujuma hiyo ya kigaidi ya Marekani.

Shahidi Qassem Soleimani 

Siku tano baada ya hujuma hiyo ya kigaidi, Iran ambayo iliahidi kulipiza kisasi cha mauaji ya Kamanda Soleimani iliipiga na kuisambaratisha kwa makombora kadhaa kambi ya kijeshi ya Ain al Assad iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani katika mkoa wa al Anbar magharibi mwa Iraq na kushambulia kambi nyingine ya kijeshi ya Marekani huko Erbil.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ilisema kuwa, shambulio hilo katika kambi ya kijeshi ya Marekani iliyopewa jina la " Oparesheni ya Shahidi Soleimani" ilikuwa pigo la awali tu na kwamba kisasi cha mauaji ya kamanda huyo "hakijamalizika." 

Kitabu kipya kilichopewa jina la "The Divider: Trump in the White House, 2017-2021" ambacho kimepangwa kuchapishwa wiki ijayo, kimeeleza kuwa, Donald Trump aliwaeleza marafiki zake akiwa katika hafla ya mchapalo (Cocktail Party) huko Florida mwezi Disemba mwaka 2020 kwamba, alikuwa akihofia kuwa Iran ingejaribu kumuuwa, kwa hiyo alipasa kuekelea Washington kwa ajili ya usalama wake. Waandishi wa kitabu hicho ni  Peter Baker na Sudan Glasser. 

Tags