Sep 15, 2022 03:14 UTC
  • Ennahda yapinga kamatakamata ya wanasiasa nchini Tunisia

Harakati ya Ennahda nchini Tunisia imelaani vikali kile ilichoeleza kuwa ni kukamatwa kiholela kwa watu kadhaa akiwemo kiongozi wa ngazi ya juu wa harakati hiyo, Habib Al-Louz na kutaka waachiliwe huru mara moja.

Harakati hiyo ilisema katika taarifa yake jioni ya jana, Jumatano, kwamba Al-Louz - mjumbe wa Baraza la Shura la harakati hiyo - alikamatwa na watu wasiojulikana na bila kuzingatia taratibu za kisheria.

Harakati hiyo imetaka kukomeshwa kwa kampeni ya kukamata watu, na kulaani kampeni za vyombo vya habari zenye nia mbaya zilizoanzishwa na baadhi pande zinazojulikana kuwa na chuki dhidi ya vuguvugu la Ennahda.

Chama cha Ennahda kimetangaza kwamba, kinachoendelea ni "jaribio jipya la kupotosha maoni ya umma kutoka kwenye masuala muhimu kama kukwama kwa matarajio na kiwango cha chini cha matumaini miongoni mwa Watunisia, na vilevile kushindwa kwa serikali ya sasa ya nchi hiyo iliyotwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi."

Taarifa hiyo imekosoa serikali ya Tunisia ikisema "imewazidishia wananchi mizigo mizito kutokana na ongezeko la bei za bidhaa na uhaba wa vyakula kama mkate, maji, maziwa, sukari na mafuta na gharama kubwa za shuleni na vyuo vikuu."

Hapo awali, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba Habib El-Louz, mbunge wa zamani na mkuu wa Chama cha Ulinganiaji na Mageuzi, alikamatwa Jumatano ya jana katika mji wa Sfax na maafisa wa Kitengo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu wa Ugaidi.

Shirika la habari la Ujerumani limenukuu chanzo kimoja katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia kikisema kuwa Al-Louz alikamatwa "katika muktadha wa uchunguzi unaoendelea kuhusu mitandao ya kuwapeleka watu nchini Syria kwa ajili ya kupigana."

Harakati ya Ennahda inakanusha madai ya kuwa na uhusiano wa aina yoyote na faili hilo, na inasema kwamba hiyo ni kampeni inayolenga kuchafua jina la chama hicho kikubwa zaidi cha upinzani nchini Tunisia. 

Tags