Sep 15, 2022 03:17 UTC
  • Wacanada hawataki kuendelea kuwa kwenye makucha ya ufalme wa Uingereza

Matokeo ya uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni yanaonesha kuwa, idadi kubwa ya wananchi wa Canada hawataki kuendelea kuwa chini ya makucha ya mfalme wao ajinabi, yaani Uingereza.

Ikumbukwe kuwa, Malkia Elizabeth II wa Uingereza alifariki dunia Alkhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 96.

Kifo cha Malkia wa Uingereza ambaye ameitawala nchi hiyo ya Ulaya kinyume na dekokrasia kwa muda wa miaka 70 yaani kuanzia mwaka 1952 hadi 2022, kimetoa fursa kwa makoloni mbalimbali ya Uingereza kuongeza harakati zao za kujitoa kwenye makucha ya mkoloni huo kizee wa Ulaya.

Karibu nusu ya kipindi cha umalkia wa Elizabeth II kilishuhudia mapambano ya mataifa ya dunia ya kujipapatua kutoka kwenye ubeberu wa Uingereza na alichobakisha nyuma malkia huyo ni urithi mchungu wa ukoloni wa Uingereza wa mamia ya miaka katika mataifa ya kona zote za dunia. 

Rangi ya kijani ni ardhi ya Canada ambayo hadi leo iko kwenye makucha ya ufalme wa Uingereza

 

Shirika la habari la IRIB limeripoti kuwa, matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa mwezi Aprili 2022 na Taasisi ya Angus Reid na kutangazwa Jumanne yanaonesha kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wa Canada hawataki kuwa chini ya makucha ya mkoloni Muingereza.

Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Leger nao unaonesha kuwa, karibu asilimia 77 ya wananchi wa Canada wanasema kuwa ufalme wa Uingereza ni ufalme wa wageni ambao hauna uhusiano wowote na wananchi wa Canada. Asilimia 87 ya wakazi wa baadhi ya majimbo ya Canada wanasema kuwa, wao hawana uhusiano wowote na ukoo wa kifalme wa Uingereza, si wa karibu wala si wa mbali na wanashangaa kwa nini nchi yao inaendelea kuwa chini ya makucha ya ufalme huo ambao unatawala kinyume na demokrasia.

Tags