Sep 16, 2022 04:01 UTC
  • Kushadidi ubaguzi dhidi ya Waislamu nchini Uingereza; kielelezo cha chuki dhidi ya Uslamu barani Ulaya

Katika muendelezo wa ubaguzi dhidi ya Waislamu wanaoishi nchini Uingereza, vyombo vya habari vimeripoti wiki hii juu ya kuweko mpango wa kupokonywa uraia wa nchi hiyo Waislamu wanaoishi nchini Uingereza na kutangazwa kuwa raia wa daraja la pili.

Taasisi ya Mahusiano ya Mbari ya Uingereza (The Institute of Race Relations) imesema, sera ya serikali ya Uingereza inawafanya Waislamu wa nchi hiyo kuwa raia wa daraja la pili kutokana na sheria zinazoruhusu kupokonywa uraia wa Uingereza. Gazeti la Uingereza la "The Guardian" limeinukuu taasisi hiyo ikisema katika ripoti yake kwamba, Sheria ya Utaifa na Ulinzi wa Mipaka, inayoruhusu kupokonywa uraia raia wanaostahili kupata uraia wa nchi nyingine, kimsingi inawalenga Waislamu, inaimarisha mizizi ya ubaguzi na kuunda uraia wa daraja ya chini kuliko ule wa Waingereza wengine.

Kadhalika ripoti ya taasisi hiyo imesema kuwa, sera za serikali ya Uingereza kimsingi zinawalenga Waingereza wenye asili ya Asia Kusini, ambao wengi wao wanatoka katika jamii ya Kiislamu.

Serikali ya wahafidhina nchini Uingereza imedai kwamba, watakaopokonywa uraia eti ni wale ambao hatua wanazozichukua zinatishia usalama wa taifa au endapo watapatikana na hatia ya kutenda jinai kubwa. Hii ni katika hali ambayo, wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, katika utendaji na utekezaji wa sheria hii kuna vigezo tata na kuna uwezekano mkubwa wa kujichukulia maamuzi na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu.

Theresa May, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza 2010-2016, Disemba 2013 aliwafutia uraia Waislamuu 20 waliokuwa wakiishi nchini humo hatua ambayo ilikuwa kinyume kabisa na kauli zake za hapo kabla. Hatua hizo za kibaguzi zilikaririwa tena na waziri aliyekuja baada yake na walengwa katika hilo walikuwa ni Waislamu wa Uingereza na siyo jamii nyingine.

 

Nukta ya kutafakari hapa ni hii kwamba, kwa raia asili wa Uingereza suala la uraia ni haki ya wazi na isiyopokonyeka na wala haina sharti hili wala lile. Lakini hali iko kinyume kabisa kwa Waingereza wengine hasa wageni waliozaliwa nchini humo au watu wengine ambao wana uraia wa kuomba, kwani huweza kupokonywa uraia huo wakati wowote.

Frances Webber, makamu mwenyekiti mtendaji wa Taasisi ya Mahusiano ya Mbari ya Uingereza (The Institute of Race Relations) anasema kwamba: "Ujumbe wa sheria hiyo inayohusiana na kupokonywa uraia tangu 2002 na utekelezaji wake, ambayo inatumiwa kwa kiasi kikubwa dhidi ya Waislamu wa Uingereza wenye asili ya Asia Kusini, ni kwamba hawa si raia halisi na hawatakuwa hivyo - licha ya kuwa na pasi za kusafiria za Uingereza -."

Weber ameongeza kuwa: "Ingawa raia wa Uingereza ambaye hana utaifa mwingine anaweza kufanya uhalifu mbaya zaidi bila kuhatarisha haki yake ya kubaki Muingereza, lakini hakuna raia wa Uingereza kati ya wale wanaoweza kupata uraia wa nchi nyingine, wanaokadiriwa kufikia milioni 6, anayeweza kujiamini kwamba atabakia na uraia wake."

Suala la chuki dhidi ya Waislamu katika madola ya Ulaya ikiwemo Uingereza limeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni. Ubaguzi huo unashuhudiwa hata katika ngazi za serikali nchini Uingereza ambapo mfano wa wazi kwa sasa ni sheria hii ya kuwapokonya uraia raia wa nchi hiyo ambayo kimsingi inawalenga Waislamu tu.

Licha ya madai ya serikali ya kihafidhina ya Uingereza kudai kwamba, inapinga mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu, lakini chama tawala nchini humo ambacho wajumbe wake ndio wanaounda serikali, kimelifanya suala la chuki dhidi ya Uislamu kuwa jambo la kawaida. Hapana shaka kuwa, utendaji wa chama tawala cha kihafidhina nchini Uingereza ndio ulioifanya serikali nayo kufuata mkondo huo na hivyo kuifanya ichukue maamuzi makali na ya kiushinikizaji zaidi dhidi ya Waislamu.

Maandamano ya chuki dhidi ya Uislamu

 

Salman Sayyid, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Leeds cha nchini Uingereza anasema: Chuki dhidi ya Uislamu zinaongezeka nchini Uingereza na sababu kuu ya hilo ni juhudi za Waislamu za kuonyesha uwepo wao katika jamii na kuonyesha utambulisho wao wa Kiislamu.

Utafiti uliofanywa na Kamati ya haki za Binadamu ya Kiislamu unaonyesha kuwa, asilimia 80 ya Waislamu nchini Uingereza wanasema kuwa, ni wahanga wa chuki dhidi ya Uislamu. Takwimu rasmi za kituo cha taifa cha nguvukazi cha Uingereza nazo zinaonyesha kuwa, Waislamu wa Uingereza ni jamii ya wachache ambayo inabaguliliwa sana katika masuala ya kazi na ajira.

Inaelezwa kuwa, Waislamu 7 kati ya 10 ambao wanafanya kazi nchini Uingereza kwa namna moja au nyingine wamekumbana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu. Aidha takwimu zinaonyesha kuwa, bahati ya Waislamu Wanaume kupata kazi nchini Uingereza ni ndogo kwa asilimia 76 ikilinganishwa na wanaume wa jamii nyingine.

Kiujumla ni kuwa, chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza kama ilivyo katika mataifa mengine ya bara Ulaya zinaendeshwa kwa mbinu na mikakati mbalimbali kama vile kuandaliwa mafaili bandia ya tuhuma dhidi ya Waislamu, kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu, propaganda chafu na kubwa dhidi ya Uislamu na Waislamu na vilevile aina kwa aina ya ubaguzi dhidi yao kama vile kuandaliwa uwanja wa kupokonywa uraia wao.

Tags