Sep 17, 2022 01:23 UTC
  • Upinzani wa marais wa Russia na China dhidi ya ulimwengu wa kambi moja

Rais wa Russia, Vladimir Putin, alisema Alkhamisi iliyopita katika mazungumzo yake na mwenzake wa China Xi Jinping yaliyofanyika kando ya mkutano wa kilele wa "Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai" huko Samarkand, nchini Uzbekistan kwamba jitihada za kuunda ulimwengu wa kambi moja hazikubalika.

Putin alisema: "Juhudi za kuunda ulimwengu wa kambo moja hivi karibuni zimechukua sura mbaya kabisa na hazikubaliwi kabisa na idadi kubwa ya nchi." Wakati huo huo, Rais wa Russia ametangaza utayarifu wa Moscow "kuwa na nafasi kubwa" katika kuielekeza dunia kwenye njia ya maendeleo endelevu na chanya. 

Kwa upande wake Rais Xi Jinping  wa China amesema dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia. Amesema, Jamhuri ya Watu wa China na mshirika wake yaani Russia, iko tayari kuonesha mfano wa kuigwa wa nchi yenye nguvu lakini inayowajibika, na kuwa na nafasi kubwa katika kujenga dunia ambao inabadilika kwa kasi kuelekea kwenye maendeleo endelevu na chanya.

Msisitizo wa marais wa Russia na China wa kupinga ulimwengu wa kambi moja umetolewa kutokana na kuendelea juhudi za kambi ya Magharibi inaoongozwa na Marekani za kutaka kudumisha sera za kiliberali duniani kwa maslahi ya nchi za Magharibi. Mfano wa juhudi hizo za kuendeleza mfumo wa kambi moja ni hatua za Washington na washirika wake kuunda miungano mbalimbali ya kijeshi na kiusalama katika eneo la Asia kwenye Bahari ya Pacific ili kukabiliana na kile kinachoitwa 'kupanuka kwa ushawishi wa China', kama vile muungano wa Quad (unaojumuisha nchi za Marekani, Australia, Japan na India) na muungano wa AUKUS (Marekani, Uingereza na Australia).

Hii ni pamoja na kuwa dunia inaelekea kwenye mfumo wa kambi nyingi kutokana na mielekeo ya kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi na kiusalama katika ngazi ya kimataifa, hasa kutoka kwa mataifa yenye nguvu kama Russia na China ambayo Washington imeyataja katika hati na nyaraka zake za kiusalama, kuwa ni nchi zinazotaka mabadiliko. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov anasema: "Marekani inatangaza hadharani kwamba inataka kudumisha milele ulimwengu wa kambi moja, ilhali hali imeshika mkondo na mwelekeo kinyume. Dunia ina kambi kadhaa."

Sergei Lavrov

Msimamo wa wazi wa Russia na China wa kupinga juhudi za Marekani kudumisha mfumo wa kambi moja umeelezwa kukabiliana na misimamo ya Rais wa Marekani, Joe Biden. Biden, ambaye anajua vyema vitendo haribifu vya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, vya kutaka kuendeleza sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika masuala ya kimataifa na kudumisha utawala wa Marekani katika mfumo wa dunia, amejaribu kwa kutumia njia nyingine, na mara hii chini ya kisingizio cha vita vya Ukraine, kuendeleza udhibiti wa Marekani duniani. Biden anaamini kwamba anawajibika kufufua nafasi ya kimataifa ya Marekani katika kipindi cha utawala wake. Kuhusiana na hilo, amesisitiza kuwa Marekani inakusudia kudumisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Indo-Pacific kwa kuunda miungano mipya, na kushikamana na Ulaya katika kampeni dhidi ya Russia. Hii ina maana kwamba Washington ina nia ya kuendeleza nafasi yake ya kujifanya polisi wa dunia. 

Kwa upande mwingine, Russia na China zimetangaza mara kwa mara kuwa licha ya kwamba Marekani bado ni nchi yenye nguvu duniani, lakini mfumo mpya wa kimataifa unaelekea kwenye dunia ya kambi kadhaa; na hapana shaka yoyote kwamba kuibuka kwa madola mapya yenye nguvu hususan China katika nyanja za kiuchumi ambayo yana uwezo wa kushindana na Marekani kwa kuzingatia viashiria kadhaa, ikiwa ni pamoja na uzalishaji ghafi wa ndani na hata yanaonekana kuanza kuitimulia kivumbi na kuiacha nyuma Marekani, kunabatilisha madai ya Washington ya kuwepo mfumo wa kambi moja. Daniel Nexon profesa wa Chuo Kikuu cha Georgetown, anasema: "Marekani lazima ikubali kwamba ulimwengu wa sasa haufanani tena na zama za kipekee na za kihistoria za miaka ya 1990 na muongo wa kwanza wa karne ya sasa. Zama za utawala wa kambi moja zimekwisha na hazitarudi."

Hali halisi ya mfumo wa sasa wa kimataifa inaonesha kuibuka kwa madola mapya yenye nguvu kama vile China, India, Russia na mataifa mengine yanayoibukia ya kiuchumi ambayo yana uwezo mkubwa. Wakati huo huo kuundwa kwa taasisi na makundi kama "BRICS" na "Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai" " kunaonesha kwamba madaraka na nguvu vinahama kutoka Magharibi kwenda Mashariki mwa dunia.

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya BRICS

Kwa hivyo, licha ya madai ya Marekani na msisitizo wake wa kutaka kuwa na nafasi muhimu ya kuongoza dunia, lakini mielekeo ya kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kiusalama ni kinyume na matakwa haya ya Washington.

Tags