Sep 23, 2022 07:03 UTC
  • Hotuba ya Biden katika Umoja wa Mataifa na lawama zisizo na msingi kuhusu masuala mbalimbali

Katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, Rais Joe Biden wa Marekani aliashiria masuala mbalimbali na kufafanua msimamo wa Washington kuhusu masuala hayo.

Moja ya masuala aliyozungumzia ni suala la haki za binadamu na hali yake katika sehemu mbalimbali za dunia, zikiwemo Iran, Afghanistan na Myanmar. Biden amedai kuwa nchi yake "daima itatetea haki za binadamu ndani ya Marekani na katika pembe za mbali kabisa duniani." Amesisitiza katika hotuba hiyo kwamba Marekani itaendelea kutetea haki ya watu wote kubainisha malalamiko yao kwa njia ya amani.

Madai ya Biden kuhusu haki za binadamu yametolewa katika hali ambayo Marekani ni mojawapo ya wavunjaji wakubwa wa haki za binadamu duniani. Licha ya nara zinazopigwa na serikali ya Marekani kuhusu kuheshimiwa haki za binadamu, kulindwa haki za mtu binafsi na za kijamii na kutetewa uhuru na haki za uraia katika nchi hiyo, lakini utendaji wa serikali ya Marekani kuhusu masuala mbalimbali kama vile unyanyasaji, unyama na ubaguzi unaotendewa wakazi asili, walio wachache, watu weusi, muamala wa kikatili dhidi ya wahamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha watoto na wazazi wao, ukatili usio na kikomo wa polisi wa Marekani dhidi ya watu wasio weupe, hali ya wafungwa, ukiukaji wa sheria za faragha na kesi nyingine nyingi, yote hayo ni mambo yanayothibitisha wazi uongo wa madai yanayotolewa na watawala wa Washington kuhusu suala zima la eti kutetea haki za binadamu.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Vahid Jalalzadeh, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran anazungumzia kesi za ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani na kusema: Idadi ya watu wa Marekani ni asilimia 5 tu ya watu wote duniani, lakini asilimia 25 ya wafungwa wote duniani wanapatikana katika magereza ya nchi hiyo. Vitendo vya mabavu na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya Walatino, wanawake, watu weusi na matabaka mengine ya jamii hushuhudiwa nchini humo kila siku, lakini Marekani inafumbia macho jambo hilo na kudai kwamba ni mtetezi wa haki za binadamu duniani.

Wakati huo huo, Washington ina rekodi mbaya sana nje ya Marekani kupitia operesheni za kijeshi na mashambulizi ya uhalifu wa kivita inazotekeleza katika nchi nyingi kama vile Vietnam, Afghanistan, Iraq na Syria na kuanzisha magereza yenye sifa mbaya kama vile gereza la Guantanamo na unyanyasaji na mateso ya kibinadamu yanayofanyika kwenye magereza hayo dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu, jambo ambalo linaonyesha wazi uongo wa madai ya Marekani kuhusu suala la kutetea haki za binadamu.

Suala jingine ambalo rais wa Marekani alilizungumzia kwa kina katika hotuba yake hiyo ni kuikosoa Russia kwa kuishambulia Ukraine. Katika sehemu ya hotuba yake, alidai kuwa Moscow imekiuka bila aibu, Hati ya Umoja wa Mataifa na kulenga msingi ulioasisi umoja huo. Huku akikosoa uamuzi wa Russia wa kuandaa kura ya maoni kwa ajili ya kuunganishwa maeneo inayoyadhibiti huko Ukrainia na ardhi yake, Biden amesema kuwa Kremlin inakusudia kukiuka haki ya Ukraine ya kuwepo kama nchi huru na kuitaka jamii ya kimataifa isimame imara katika kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uchokozi wa kigeni. Rais wa Marekani pia amesisitiza juu ya kuwajibishwa Russia kuhusiana na uhalifu wowote wa kivita unaoweza kutokea nchini Ukraine.

Biden amekosoa uvamizi wa Russia nchini Ukraine, bila kujali rekodi ya Marekani yenyewe ya uingiliaji wake ulioandamana na umwagaji damu na maafa katika sehemu zingine za ulimwengu katika miaka themanini iliyopita. Wakati wa Vita Baridi, Marekani ilihusika na uvamizi na mashambulizi mbalimbali, muhimu zaidi ikiwa ni Vita vya Vietnam. Katika zama za baada ya Vita Baridi, baada ya Septemba 11, 2001, Marekani iliishambulia Afghanistan kwa kisingizio cha mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi na Iraq kwa kisingizio cha kuwa na silaha za maangamizi makubwa na kuua maelfu ya watu wasio na hatia.

Uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan

Baada ya hapo, utawala wa Obama tokea mwaka 2011 uliyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi nchini Syria na kwa kutoa misaada mikubwa ya kifedha, vifaa na silaha kwa makundi hayo, ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ambavyo vilipelekea mamia kwa maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha. Aidha, Washington imeendeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani tangu uongozi wa George W. Bush kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu katika sehemu mbalimbali za dunia. Kwa kuzingatia hayo, rais wa Marekani, akiwa kiongozi wa nchi ambayo imekuwa ikichochea zaidi vita na umwagaji damu duniani, sasa amejipa haki ya kudai kutetea haki za Waukraine na kuikosoa Russia kuhusu suala hilo. Hii ni katika hali ambayo Marekani na washirika wake wa Ulaya ndio wahusika wakuu wa kuendelea kupanuka vita vya Ukraine kwa kuipa nchi hiyo mabilioni ya dola za misaada ya kijeshi na silaha.

Tags