Sep 23, 2022 09:34 UTC
  • Wahajiri zaidi ya 150 wanusurika kifo baada ya kutelekezwa kwenye kontena nchini Mexico

Polisi nchini Mexico wamesema kuwa wamegundua lori moja la kubeba makontena ambalo lilikuwa limetelekezwa pembeni mwa barabara moja kuu likiwa na wahajiri haramu 153.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, polisi wa jimbo la Chiapas la kusini mwa Mexico wamesema kuwa, kontena hilo na lori lake lilikuwa na raia 144 wa Guatemala, raia 6 wa Nicaragua na raia 3 wa El Salvador.

Lori hilo lilikuwa na namba ya Mexico City na lilikuwa limetelekezwa katika Baraba Kuu ya Federali ya kusini mwa Mexico. Wahariji hao haramu wamepatikana wakiwa katika hali mbaya sana na kama jeshi la polisi lisingeligundua lori hilo, kuna uwezekano mkubwa wote wangepoteza maisha.

Malori kama haya yanatumiwa sana kufanya magendo ya binadamu

 

Wahajiri hao waliookolewa na jeshi la polisi la Mexico walikuwa wanaelekea kwenye mpaka wa Marekani. Wamepewa misaada ya matibabu na saikolojia na baadaye kukabidhiwa kwa maafisa wa uhamiaji wa Mexico.

Zaidi ya wahajiri milioni 2 waliingia Marekani mwezi uliopita wa Oktoba kwa kutumia njia za panya kwenye mpaka mrefu wa Marekani na Mexico. Idadi hiyo ya wahajiri walioingia Marekani kimagendo imevunja rekodi ya mwaka uliopita wakati huu wa urais wa Joe Biden huko Marekani.

Wimbi hilo kubwa la wahamiaji haramu limewaweka kwenye wakati mgumu viongozi wa nchi mbili za Mexico na Marekani na hasa viongozi wa majimbo ya mpakani na inaonesha wazi kwamba hawana uwezo wa kudhibiti wimbi hilo.