Sep 25, 2022 03:07 UTC
  • Canada yadai haiwezi kulipa wafanyakazi wa mgodi wa Burkina Faso licha ya kunufaika nao kupindukia

Kampuni ya Trevali ya Canada inayomiliki mgodi wa Perkoa wa kuchimba madini ya zinki nchini Burkina Faso umesema kuwa umeamua kufunga mgodi huo kufuatia mafuriko mabaya yaliyosababisha vifo vya wafanyakazi wanane.

Wachimba migodi hao wanane walizama katika njia za chini ya ardhi za mgodi huo ulioko kwenye jimbo la Sanguie baada ya mvua kubwa isiyotarajiwa ya wakati wa kiangazi kunyesha katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mgodi huo ni mkubwa sana kiasi kwamba unahesabiwa kuwa ni miongoni mwa milki tatu kuu za shirika la Trevali la Canada licha ya kuweko kwake nje ya nchi hiyo ya Magharibi. 

 

Mgodi huo wa Perkoa unaendeshwa na taasisi ya Nantou Mining ya shirika la Treval la Canada. Taasisi hiyo imekuwa ikifanya juhudi za kuukarabati mgodi huo bila ya mafanikio kwa kile kinachodaiwa ni ukosefu wa fedha, licha ya kwamba dola la Magharibi la Canada linaingiza fedha nyingi sana kutoka kwenye mgodi huo wa barani Afrika.

Diti Moussa Paleinfo, mkurugenzi wa taasisi ya Nantou Mining amesema, fedha zilizopo ni kidogo na hazitoshi kukamilisha ukarabati wa mgodi huo. Pia amesema: "Fedha zilizopo hazitoshi pia kugharamia malipo ya kufukuzwa kazi wafanyikazi walioachishwa kazi kwa lazima." Hii ni katika hali ambayo, Canada imefaidika mno na madini ya zinki ya mgodi huo lakini sasa inadai haina fedha za kuukarabati mgodi huo wala kuwalipa wafanyakazi.

Wiki iliyopita, mahakama moja nchini Burkina Faso ilitoa hukumu dhidi ya watendaji wawili wa kampuni hiyo ya Canada baada ya kuwapata na hatia ya kusababisha vifo vya wafanyakazi wanane wa mgodi huo.