Sep 26, 2022 03:05 UTC
  • Ukosoaji wa Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusu kuenezwa chuki dhidi ya Waislamu

Waziri Mkuu wa Pakistan ametaka kukomeshwa mara moja chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, hasa nchini India.

Shahbaz Sharif, Waziri Mkuu wa Pakistan, amesema katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwamba chuki dhidi ya Uislamu limekuwa suala la kimataifa, na kwamba mfano wa wazi zaidi katika uwanja huo ni yale yaliyowapata Waislamu wa India katika eneo la Kashmir. Sharif ameongeza kwamba watu wa Kashmir wanapaswa kuruhusiwa kujiainishia mustakbali na hatima yao.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Waziri Mkuu wa Pakistan, amesema: "Nchi yangu inakabiliwa na maafa makubwa yanayotokana na hali ya hewa, na kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kutoa misaada ya kitaifa kwa mamilioni ya wahanga wa mafuriko."

Maneno ya Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusiana na onyo la kuenea chuki dhidi ya Uislamu ndio wasiwasi muhimu zaidi wa Waislamu katika ngazi ya kimataifa kwa sasa, ikizingatiwa kuwa hali hiyo imesababisha ongezeko la kutisha la vitendo vya ukatili dhidi ya umma wa Kiislamu katika nchi mbalimbali.

Waislamu wa India walalamikia dhulma inayofanywa na serikali dhidi yao

Tangu mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani, serikali ya nchi hiyo na washirika wake wa Magharibi, kwa kisingizio cha kuhusika al-Qaeda na Taliban katika mashambulizi hayo, walianzisha hujuma na sera kali za chuki dhidi ya Uislamu kwa shabaha ya kuwashinikiza katika nchi tofauti na hasa za Magharibi.

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, serikali ya Marekani imekuwa ikitumia visingizio tofauti na kuyanasibisha makundi ya kigaidi na Uislamu kwa lengo la kueneza chuki na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu.

Matamshi ya Shahbaz Sharif ya kukosoa siasa za nchi za Magharibi katika kueneza chuki dhidi ya Uislamu, katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yanaonyesha kuwa nchi za Kiislamu zimekasirishwa sana na kuendelea siasa hizo na kulichukulia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa fursa nzuri ya kubainishwa hofu na wasi wasi mkubwa walionao Waislamu kuhusu matokeo ya kuenezwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu katika ngazi za kimataifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, moja ya hatua zilizozidisha chuki dhidi ya Uislamu ni uamuzi wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump wa kupiga marufuku safari za raia wa nchi tano za Kiislamu kwenda Marekani, jambo ambalo lilichochea fikra za chuki dhidi ya Uislamu na kupata nguvu magenge ya chuki dhidi ya jamii ya Waislamu.

Sehemu ya hotuba ya Waziri Mkuu wa Pakistan katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilihusu mwenendo hatari wa chuki dhidi ya Waislamu na hali ya kusikitisha ya jamii ya Kiislamu nchini India, ikiwa ni pamoja na eneo la Kashmir, ambalo kwa bahati mbaya katika miaka ya hivi karibuni limekumbwa na matatizo mengi na ukatili wa kupindukia kutoka kwa magenge ya Wahindu wenye itikadi kali zisizo na msingi.

Katika miaka ya karibuni, chama tawala nchini India chenye siasa za kibaguzi dhidi ya Waislamu kimewachochea Wahindu wenye misimamo mikali kuzidisha vitendo vyao vya chuki dhidi ya Waislamu ikiwemo kuharibiwa maeneo yao matakatifu ya kufanyia ibada na kuzidisha mateso dhidi yao katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Behrouz Ayaz, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema,

Serikali ya India imehatarisha usalama wa Waislamu wa nchi hiyo ili kuwafukuza katika nchi yao na kuwalazimisha kuhamia katika nchi nyingine. Vyama vya Kitaifa, kikiwemo chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP), pia vinachochea vurugu dhidi ya Waislamu kama msingi wa kudhamini nguvu na uhai wao wa kisiasa.

Waislamu wakishambuliwa na magenge ya Wahindu wenye misimamo mikali ya chuki

Kuzuia na kubana marasimu ya kidini ya Waislamu, kuwanyima wahamiaji Waislamu vibali vya kuishi nchini, kufutwa utawala wa ndani wa Kashmir na kunyamazia mashambulizi na ukatili unaofanywa na Wahindu wenye chuki kali dhidi ya Waislamu ni miongoni mwa masuala ambayo yamechohea kuongezeka pakubwa chuki dhidi ya Waislamu wa India.

Licha ya nchi za Magharibi kukataa kukomesha chuki dhidi ya Uislamu, lakini nchi za Kiislamu zina suhula mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kibiashara za kuweza kukomesha siasa hizo za chuki dhidi ya Waislamu katika nchi mbalimbali, lakini pamoja na hayo la kusikitisha ni kuwa nchi hizo zimepuuza kabisa suhula hizo muhimu na kutozifanyia kazi kama inavyopaswa.

Tags