Sep 26, 2022 03:34 UTC
  • Papa awataka Waitaliano wazaliane kwa wingi, wawapokee wahajiri

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewatolea mwito Waitaliano wazae watoto zaidi na kuwapokea wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Papa alitoa wito huo jana Jumapili mwishoni mwa kongamano la makanisa ambalo kufanyika kwake kumesadifiana na kufanyika uchaguzi mkuu wa Italia.

Katika ujumbe aliotoa kwenye kongamano hilo, kiongozi wa Kanisa Katoliki amezungumzia pia kadhia ya wahajiri, ambayo ni moja ya ajenda kuu za kampeni za uchaguzi unaofanyika nchini humo.

Katika kongamano hilo la makanisa lililofanyika kwenye eneo la wazi katika mji wa Matera kusini mwa Italia, si Papa Francis wala wenyeji wake waandaaji wa kongamano waliogusia suala la uchaguzi katika hotuba zao, ingawa mkutano wa maaskofu wa Italia hapo awali ulikuwa umewahimiza Waitaliano kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi ambao unaweza kupelekea Italia kuongozwa na serikali ya kwanza ya mrengo wa kulia wenye misimamo mikali tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Akizungumza mwishoni mwa ibada maalumu Papa Francis aliwahimiza Waitaliano kuzaa watoto zaidi. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesema: "Nataka niiombe Italia: wazaliane zaidi, wawe na watoto zaidi".

Italia ni moja ya nchi zenye kiwango cha chini zaidi cha watoto wanaozaliwa duniani; na Papa Francis amekuwa akieleza mara kwa mara kusikitishwa na kile alichokiita "msimu wa baridi wa idadi ya watu."

Giorgia Meloni

Katika kampeni za uchaguzi, kiongozi wa mrengo wa kulia Giorgia Meloni, ambaye amefanya kampeni kwa kauli mbiu "Mungu, Familia na Nchi", ametoa wito kwa Waitaliano kubadili mwelekeo wao wa idadi ya watu huku akitangaza kutoa motisha zaidi za kifedha kwa wanandoa kwa ajili ya kuzaa watoto zaidi.

Katika hotuba yake, Papa Francis amezungumzia pia maudhui muhimu nchini Italia, ambapo sambamba na kukumbusha kuwa Jumapili ya jana imesadifiana na Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji na Wakimbizi ya Kanisa Katoliki, ametoa wito wa kufikiwa mustakabali ambao "Mpango wa Mungu" utatekelezwa; na wahamiaji na wahanga wa biashara haramu ya binadamu wataishi kwa amani na heshima na kuwa na "mustakabali wa ushirikishwaji zaidi na wa kindugu".../