Sep 26, 2022 08:20 UTC
  • Kombora jipya la Korea Kaskazini na kiwingu kizito cha vita Kusini Mashariki mwa Asia

Hatua ya Korea Kaskazini ya kufanyia majaribio kombora lake jipya kuelekea upande wa Bahari ya Japan imepokewa kwa hisia kali na nchi mbili za Japan na Korea Kusini.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida alikuwa ametangaza hali ya tahadhari kwa wizara na idara zote za nchi hiyo kabla ya kufanyiwa majaribio kombora jipya la Korea Kaskazini. Jumapili, tarehe 25 Septemba yaani muda mfupi kabla ya Korea Kaskazini kufanyia majaribio kombora lake jipya, Kishida alisema kuwa, ameamua kutangaza tahadhari maalumu kwa wizara na idara za serikali ya nchi hiyo kama njia ya kuimarisha usalama wa vyombo vya baharini na angani vya kiraia vya eneo hilo.  Pia alisema, hiyo ni katika muendelezo wa kutoa taarifa za haraka na za kuaminika kwa jamii ili iwe rahisi kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza. Vile vile Ofisi ya Waziri Mkuu wa Japan imeunda kamati maalumu ya mgogoro yenye jukumu la kukusanya, kuchambua na kutoa taarifa kwa ajili ya kukabiliana na hali iliyojitokeza baada ya jaribio la kombora jipya la Korea Kaskazini. Jeshi la Korea Kusini nalo mapema Jumapili asubuhi lilitangaza kuwa: Jirani yetu wa kaskazini amefyatua kombora lisilojulikana la balestiki kueleka upande wa Bahari ya Mshariki (Bahari ya Japan).

Tangu tarehe 24 Septemba, viongozi wa Korea Kusini walikuwa wametangaza kuwa, wameiweka nchi katika hali ya tahadhari kutokana na kuweko taarifa kwamba Korea Kaskazini ina nia ya kufanyia majaribio kombora la balestiki kutoka kwenye nyambizi. Wakati huo huo afisa mmoja wa kijeshi wa Korea Kusini alisema: Tunazifuatilia kwa karibu harakati za taasisi za makombora za Korea Kaskazini na tumejiandaa kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.

Kombora la nyuklia la Korea Kaskazini

 

Korea Kaskazini imefanyia majaribio kombora lake la masafa mafupi kuelekea upande wa Bahari ya Japan katika hali ambayo madola ya kibeberu na hasa Marekani nayo yamezidisha uchochezi wao kwenye maeneo yenye hali tete na mzozo ya kusini mashariki mwa Asia. Kiujumla ni kwamba Korea Kaskazini inaonesha kivitendo kuwa imejiandaa vilivyo kukabiliana na hali yoyote dhidi yake hasa kutokana na uchochezi unaofanywa na madola ya kiistikbari kwa kuwatumia waitifaki wao wa kusini mashariki mwa Asia kama vile Korea Kusini na Japan.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, Korea Kaskazini imefanya majaribio yasiyopungua 18 ya silaha zake huku sehemu kubwa ya majaribio hayo ikiwa ni kufyatua makombora yake ya balestiki. Majaribio hayo yanaonesha kuongezeka idadi ya silaha za nyuklia na makombora ya nchi hiyo. Hii ni kusema kuwa mbali na kutia nanga manuwari nyingi za Marekani katika eneo la kusini mashariki mwa Asia, lakini moja ya hatua za kichochezi za nchi za Maghairibi hasa Marekani katika eneo hilo hatari ni kufanya maneva ya kijeshi katika fukwe za Japan na Korea Kusini. Kuweko manuwari za kivita za Marekani katika eneo tete na lenye mizozo la kusini mashariki mwa Asia kuna maana kwamba, tawala zenye fikra za Magharibi za nchi za eneo hilo zinasubiri fursa tu ya kuingia vitani na Korea Kaskazini. Inaonekana wazi pia kuwa, nchi mbili za Marekani na China zimeamua kuzitumia nchi nyingine kama chambo cha kuongezeana mashinikizo Washington na Beijing hususan kwa vile China inahesabiwa kuwa ni muitifaki wa Russia katika eneo la kusini mashariki mwa Asia huku nchi kama Japan na Korea Kusini zikiwa waitifaki wa karibu wa Marekani.

 

Alaakullihaal, ni vyema tuseme hapa kwamba, Korea Kaskazini imefanyia majarfibio kombora lake jipya la masafa mafupi la balestiki siku chache tu baada ya Marekani kupeleka manuwari yake kubwa ya kubebea ndege za kivita katika fukwe za Korea Kusini kwa ajili ya kile kilichodaiwa na dola hilo la kibeberu kuwa ni kufanya luteka ya pamoja ya kijeshi na Korea Kusini. Korea Kaskazini imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba: Inaimarisha na kutia nguvu uwezo wake wa kijeshi kadiri inavyoweza kutokana na hatua za kichochezi za Marekani katika eneo hili na hatua yake ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara ya kijeshi na vibaraka wake karibu na mipaka ya Korea Kaskazini.

Amma kwa upande wao, wataalamu mbalimbali wa masuala ya kijeshi wanasema kuwa, Marekani na waitifaki wake wameingiwa na wasiwasi na woga mkubwa kutokana na majaribio ya mara kwa mara ya silaha mpya za Korea Kaskazini, suala ambalo ni ushahidi tosha kuwa Pyongyang ina silaha nyingi zisizojulikana zikiwemo za nyuklia za kuweza kukabiliana na maadui zake.

Tags