Sep 26, 2022 11:02 UTC
  • 13 wauawa, 21 wajeruhiwa katika shambulio la ufyatuaji risasi kwenye skuli moja ya Russia

Polisi ya Russia imetangaza kuwa watu 13 wameuawa na wengine 21 wamejeruhiwa katika shambulio la ufyatuaji risasi lililotokea kwenye skuli moja kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, polisi ya mji wa Izhevsk, ulioko katika Jamhuri ya Udmurtia kusini mwa Russia imetangaza kuwa  shambulio hilo la ufyatuaji risasi limetokea leo katika skuli moja ya mji huo.
Gavana wa Udmurtia, Alexander Berchalov amesema mshambuliaji, kwanza alimuua mlinzi wa skuli na baada ya kufanya mauaji, akajiua mwenyewe.
Inasemekana mhusika wa shambulio hilo alikuwa amevalia fulana nyeusi yenye nembo za Kinazi, ingawa hadi sasa utambulisho wake haujafahamika na sababu ya kufanya shambulio katika skuli hiyo bado haijajulikana.
Kamati ya Uchunguzi ya Russia imetangaza kuwa watu wasiopungua wanane miongoni mwa waliouawa ni wanafunzi wa skuli hiyo ya mji wa Izhusk.
Kamati hiyo imeongeza kuwa, walinzi wawili na walimu kadhaa pia waliuawa katika shambulio lililopelekea kujeruhiwa pia watu 21, wakiwemo watoto 14.
Polisi ya Russia imetangaza kupatikana mwili wa mshambuliaji wa skuli hiyo ambaye inavyoonekana alichukua hatua ya kujiua. Mamlaka husika zimeeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo ungali unaendelea.
Izhusk ni mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika shirikisho la Russia ambapo watu wapatao laki sita na elfu 30 wanaishi katika mji huo. Mji huo uko karibu na milima ya Ural inayotenganisha mabara ya Ulaya na Asia.../

Tags