Sep 27, 2022 02:12 UTC
  • Kuongezeka maradufu bajeti ya kijeshi ya UK, kushiriki London kwenye chokochoko za kijeshi za Washington

Licha ya Uingereza kukumbwa na mgogoro wa kiuchumi baada ya janga la corona na kupungua thamani ya sarafu ya nchi hiyo, lakini London imeamua kuongeza maradufu bajeti yake ya matumizi makubwa ya kijeshi.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace, alisema juzi Jumapili tarehe 25 Septemba 2022 kwamba, nchi hiyo ya Ulaya imeamua kuongeza maradufu matumizi yake ya kijeshi kwa sababu ya vita vya Ukraine.

Amesema, London itaongeza pound bilioni 52 (sawa na dola bilioni 56.5 za Kimarekani) kwa ajili ya kujiimarisha kijeshi. Mpango huo unaendana na kaulimbiu ya uchaguzi ya waziri mkuu mpya wa Uingereza, Liz Truss. Wakati wa kampeni za kupigania kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Truss alisema kuwa, ataongeza bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo na kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 bajeti hiyo inafikia pound bilioni 100. Aidha katika hotuba yake kwenye kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Liz Truss alisema, ifikapo mwaka 2030 atahakikisha kuwa asilimia 3 ya pato la uzalishaji wa malighafi wa Uingereza linakwenda kwenye matumizi ya kijeshi. Vile vile Truss amesimamisha mpango wa waziri mkuu aliyepita wa Uingereza, Boris Johnson, wa kupunguza wanajeshi 9,500 kutoka kwenye vikosi vya ulinzi ya nchi hiyo.

Ben Wallace (katikati)

 

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amedai kuwa, nchi hiyo imezoea kuwa na upungufu wa bajeti yake ya kijeshi kwa miaka 30 hadi 40, lakini sasa inabidi izoee kuwa na utamaduni mwingine wa kijeshi.

Inaonekana wazi kwamba, kuongezwa maradufu bajeti ya kijeshi ya Uingereza licha ya jamii ya nchi hiyo kuishi kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi hivi sasa, ni katika juhudi za London za kuwa pamoja na Marekani katika chokochoko zake za kijeshi huko barani Ulaya na katika maeneo mengine ya dunia. Pia ni kujaribu kuonesha kuwa Uingereza bado ina nguvu na ushawishi wa kijeshi licha ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Aidha inaonekana wazi kuwa London imo katika kukabiliana na madola mengine yenye nguvu na haitaki kubaki nyuma katika siasa za Ulaya kuhusu nchi kama Russia na China.

Baada ya kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya miaka miwili iliyopita, muda wote Uingereza imekuwa kwenye mchakato wa kujipanga upya na kulinda nafasi yake barani Ulaya na duniani kwa ujumla. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na London katika uwanja huo ni kuanza kutumia manuwari mpya mbili za kubeba ndege. Hata hatua yake hii ya kuongeza maradufu bajeti yake ya kijeshi, inahesabiwa kuwa imechukuliwa katika uwanja huo huo. Kitendo cha London cha kujiunga na muungano wa Aukus unaoundwa na Marekani, Uingereza na Australia kwa ajili ya kukabiliana na kile kinachodaiwa kujitanua China, pia kinahesabiwa kuwa ni katika mchakato huo wa Uingereza wa kujipanga upya baada ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Zaidi ya yote ni kwamba, Uingereza iko bega kwa bega na Marekani katika kuimiminia silaha Ukraine kwa ajili ya kukabiliana na Russia. Nchi hizo mbili za Magharibi ndizo zinazoirundikia zaidi silaha Ukraine kuliko nchi zote za Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Uingereza amesema: Uhusiano wetu na Marekani ni wa kipekee na uhusiano huo unazidi kuwa na umuhimu wakati tunapokabiliwa na vitisho vya Russia na kuongezeka nguvu za China.

Liz Truss, waziri mkuu mpya wa Uingereza mwenye misimamo mikali ya kutumia nguvu za kijeshi

 

Pamoja na yote hayo swali linalojitokeza hapa ni kwamba, je, uamuzi wa serikali ya kihafidhina ya Liz Truss huko Uingereza, wa kuongeza maradufu bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo unaendana na hali halisi ilivyo ya kimaisha ya nchi hiyo? Serikali hiyo ya waziri mkuu mpya wa Uingereza imeamua kuongeza mno matumizi ya kijeshi katika hali ambayo madeni ya serikali ya London ni makubwa mno hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi hiyo ya Ulaya. Mfumuko wa bei na kupanda vibaya gharama za maisha na hasa bei za chakula na nishati, ni mambo ambayo hayaendani na uamuzi wa Uingereza wa kudharau matatizo makubwa ya wananchi na kuamua kutumia fedha nyingi katika kushiriki kwenye chokochoko za kijeshi za Marekani. Imani ya wananchi wa Uingereza imeporomoka mno katika kipindi cha miongo kadhaa sasa, kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa nchi hiyo ya Ulaya Magharibi hawana tena matumaini ya kuwa na mustakbali bora katika siku za usoni.

Tags