Sep 27, 2022 08:08 UTC
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka kukomeshwa vitisho vya nyuklia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kukomeshwa vitisho vya nyuklia na badala yake watu wajitolee kwa ajili ya kudumisha amani duniani.

Antonio Guterres amesema hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kabisa Silaha za Nyuklia, hafla iliyofanyika huku mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukifikia tamati.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, silaha za nyuklia ndizo nguvu za uharibifu zaidi kuwahi kuundwa. Hazileti usalama wowote, ni mauaji na machafuko tu. Kuondolewa kwazo kungekuwa zawadi kuu tunayoweza kutoa kwa vizazi vijavyo.

Guterres amekumbushia kwamba Vita Baridi vilileta wanadamu “ndani ya dakika chache za maangamizi.” Hata hivyo miongo kadhaa baada ya kumalizika, na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, "tunaweza kusikia tena mlio nyuklia." 

Niweke wazi. Enzi ya vitisho vya nyuklia lazima iishe.

Aidha Katibu Mkuuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya kuwa na maono mapya ya kutokomeza silaha za nyuklia akiashiria Ajenda yake Mpya ya Amani ambayo inatoa wito wa kupokonya silaha na kuendeleza uelewa wa pamoja wa vitisho vingi vinavyoikabili jamii ya kimataifa.

"Tunahitaji kuzingatia utaratibu wa nyuklia unaoendelea, ikiwa ni pamoja na aina zote za silaha za nyuklia na njia zao za usambazaji. Na tunahitaji kushughulikia mistari yenye ukungu kati ya silaha za kimkakati na za kawaida, na uhusiano na nyanja mpya za mtandao na anga za juu. " Amesisitiza Guteres.