Sep 28, 2022 04:49 UTC
  • Majimbo ya Ukraine yapiga kura ya kujiunga na Russia katika siku ya mwisho ya kura ya maoni

Raia katika majimbo mawili yaliyotangaza kujitenga na Ukraine mashariki mwa nchi hiyo ya Luhansk na Donetsk na pia maeneo ya Kherson na Zaporizhia yanayodhibitiwa na Russia jana Jumanne walishiriki katika kura ya maoni ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo.

Leonid Pasechnik Kiongozi wa Jamhuri ya watu wa Luhansk jana Jumanne alipiga kura yake ya maoni. Kura hiyo ya maoni iliyoanza Ijumaa ilipangwa kumalizika jana jioni. Pasechnik amesema kuwa, amepiga kura ya kujiunga na Russia baada ya miezi saba ya  kupamba moto vita kati ya Moscow na Kiev. Huku hayo yakiarifiwa, serikali ya Kiev ilikuwa imewatahadharisha wakazi wa majimbo hayo ikisema kuwa atakayeshiriki kwenye kura hiyo ya maoni atakabiliwa na kesi ya uhaini.

Majimbo ya Luhansk na Donetsk 

Mikhailo Podolyak Mshauri wa Rais wa Ukraine alisema kuwa, wanayo majina ya watu walioshiriki katika kura hiyo ya maoni kwa kiwango fulani. "Tunazungumzia juu ya mamia ya watu waliofanikisha zoezi hilo. Watu hao watahuklumiwa kwa kosa la uhaini." Mshauri huyo wa Rais wa Ukraine hata hivyo amesema kuwa: raia wa Ukraine ambao inasemekana wamelazimishwa kupiga kura hawataadhibiwa. 

Rais Vladimir Putin wa Russia pia ameunga mkono kura hiyo ya maoni ambayo imekosolewa na nchi za Magharibi ambapo wameitaja kuwa ni fedheha. Nchi hizo zimeapa kutotambua matokeo ya kura hiyo ya maoni. Kura ya maoni kwa ajili ya kujiunga na Russia majimbo ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhia imefanyika huku mapigano yakiendelea kati ya majeshi ya Ukraine na yale ya Russia. 

Tags