Sep 28, 2022 10:45 UTC
  • Moscow: Marekani inaichochea Russia itumie silaha za nyuklia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, Marekani inafanya vituko ambavyo vinaonesha wazi kuwa lengo lake ni kuichochea Russia itumie silaha za nyuklia.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo leo na kumnukuu Maria Zakharova akisema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na redio moja na kuongeza kuwa: "Washington haichungi mipaka yoyote katika kufanya vituko na chokochoko zake. Inatumia njia zote za vita kwa ajili ya kuisukuma Moscow kwenye kutumia silaha za atomiki."

Amesisitiza kwa kusema: "Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba lengo lao (Wamarekani) ni uharibifu tu."

Maria Zakharova

 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amegusia pia jinsi Moscow inavyoendesha mambo yake kwa busara na tahadhari kubwa na jinsi ilivyotangaza mara chungu nzima kuwa iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani na kusema: Juhudi zote hizo za Russia zinafanyika lakini Marekani inakwamisha mambo bali inachukua hatua mbaya zinazolenga kuzusha maafa na balaa dunia nzima.

Ikumbukwe kuwa uamuzi wa mwisho wa kutumia silaha za nyuklia kwa mujibu wa katiba ya Russia umo mikononi mwa rais wa nchi hiyo ambaye hivi sasa ni Rais Vladimir Putin.

Rais wa zamani wa Russia, Dmitry Medvedev hivi karibuni alizionya nchi za Ulaya na Marekani akisema kuwa, kwa mujibu wa stratijia za kiulinzi za Russia, Moscow ina haki ya kujihami kwa silaha zozote zile zikiwemo za atomiki.

Tags