Sep 29, 2022 02:25 UTC
  • Waingereza weusi wakosoa ubaguzi wa rangi katika sekta ya afya

Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa Waingereza wengi weusi (wenye asili ya Afrika) wanalalamikia mienendo ya kibaguzi ya wataalamu wa afya nchini humo.

Mtandao wa Independent umeripoti kuwa, kulingana na matokeo ya uchunguzi wa kitaifa, asilimia 75 ya Waingereza weusi wenye umri wa kati ya miaka 18 na 34 wamekumbana na mienendo ya ubaguzi wa rangi wanapotembelea madaktari na hospitali.

Wakati huo huo, ripoti zinaonesha kuwa, asilimia 65 ya watu wote weusi wanaoishi Uingereza wamekumbana na mienendo hiyo ya kibaguzi.

Utafiti huo umefanyika kwa wito wa Jumuiya ya Usawa wa Watu Weusi, shirika la kitaifa la kutetea haki za kiraia ambalo lilizinduliwa mapema mwaka huu (2022) ili kukabiliana na ubaguzi wa kimfumo nchini Uingereza.

Dame Vivian Hunt, rais wa Shirika la Usawa wa Weusi, amesema: "Ufunguo wa mabadiliko ni kutambua na kuelewa ukweli na hali halisi wa jumuiya za watu weusi kote nchini Uingereza."

Shirika hilo limetoa wito wa kukomeshwa "maamuzi ya chuki yaliyofanywa na wataalamu wa afya wakati wa kuwashughulikia wagonjwa weusi."

Kamati ya Pamoja ya Bunge ya Haki za Kibinadamu nchini Uingereza ilitangaza Novemba 2021 kwamba zaidi ya asilimia 60 ya watu weusi nchini Uingereza hawapewi huduma za afya na matibabu kama watu weupe.

Matokeo ya utafiti huo pia yanaonyesha ukosefu mkubwa zaidi wa usawa katika sekta ya umma.