Sep 29, 2022 02:26 UTC
  • Ukosoaji wa China kwa vikwazo vya Marekani vinavyosababisha masaibu kwa nusu ya watu wote duniani

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeikosoa Marekani kwa kutekeleza sera ya vikwazo na kusababisha matatizo na masaibu kwa nusu ya watu wote duniani.

Wang Wenbin, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amezungumzia vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya karibu nchi 40 na kusema: vikwazo vimesababisha maafa makubwa ya kibinadamu kwa nusu ya watu duniani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameashiria jinsi hatua za Marekani za kutekeleza vikwazo zilivyokosolewa na kulaaniwa vikali na viongozi wa nchi nyingi wakati walipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwemo viongozi wa Iran, Zimbabwe, Bolivia na Cuba na akaongeza kuwa: "bila shaka yoyote, Marekani, ndilo dola kuu la vikwazo duniani." Wenbin amesisitiza pia kuwa, vikwazo vilivyowekwa na Washington vimepelekea kuzuka maafa makubwa ya kibinadamu duniani.
Wang Wenbin

Kuhusu athari hatarishi zinazosababishwa na vikwazo haramu vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi kadhaa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amesema, sera ya Marekani -ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na iliyo dhidi ya ubinadamu ya kuziwekea vikwazo nchi zenye misimamo isiyoendana na siasa za Washington na zinazopinga uchu wa kujivutia kila kitu ilionao Ikulu ya White House- ni hatua ya kidhalimu, ambayo imesababisha migogoro kutokana na upinzani uliopo katika uga wa kimataifa.

Serikali ya Marekani imetumia visingizio mbalimbali kuziwekea vikwazo haramu baadhi ya nchi duniani, jambo ambalo limesababisha wananchi wa nchi hizo kukabiliwa na matatizo mengi na makubwa.
Iran ni miongoni mwa nchi ambazo zimewekewa vikwazo vikali zaidi na serikali ya Marekani kwa kisingizio cha kadhia ya nyuklia.
Mbali na kuziwekea vikwazo sekta za fedha, biashara, viwanda na nishati, Ikulu ya Marekani imejumuisha pia sekta ya dawa katika orodha yake ya vikwazo dhidi ya Iran na nchi nyingine kadhaa, jambo ambalo limegharimu maisha ya wagonjwa wengi wanaotegemea dawa zinazoagizwa kutoka nchi nyingine. 

Athari za vikwazo vya dawa za Marekani kwa nchi zilizowekewa vikwazo hivyo ikwemo Iran, hasa tangu lilipoanza janga la dunia nzima la corona hadi sasa, zimekuwa na madhara makubwa na haribifu kwa watu wa nchi hizo.

Ili kuvifanya vikwazo dhidi ya nchi ilizozilenga viwe na athari hasi ilizozikusudia, Marekani imejaribu pia kutumia mbinu ya vitisho na ya kuzirubuni nchi nyingine zikiwemo za washirika wake wa Magharibi, ziungane nayo katika kutekeleza hatua hizo za kikatili na kidhalimu, jambo ambalo kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China limesababisha maafa makubwa duniani.
Marekani imezitishia nchi nyingine na makampuni makubwa kwamba, endapo zitakiuka vikwazo ilivyoziwekea nchi nyingine itaziadhibu vikali, ambayo ni ishara nyingine ya mielekeo ya kibabe na utumiaji mabavu ya White House katika uga wa kimataifa.
Profesa Alena Douhan, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa, analizungumzia suala hilo kwa kusema:
 Alena Douhan

Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu katika upatikanaji wa watu chakula kinachostahiki na dawa. Serikali ya Marekani inapasa isimamishe vikwazo dhidi ya Iran; na Umoja wa Mataifa inapasa itoe ushirikiano wa kuanzisha utaratibu wa kufidia hasara na madhara wanayopata wahasiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu unaosababishwa na hatua za mabavu za upande mmoja.

Katika hatua yake mpya ya kuendeleza sera yake ya vikwazo, serikali ya Marekani inataka kufanya mashauriano na nchi tofauti za Ulaya na Asia kwa lengo la kushadidisha vikwazo dhidi ya Russia, jambo ambalo bila shaka litawaathiri zaidi raia wa nchi hiyo. Safari ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris huko Japan na Korea Kusini imefanyika kwa lengo hilo hilo la kuzishawishi nchi hizo zijiunge na kampeni hiyo ya kushadidisha vikwazo dhidi ya Moscow.../

 

Tags