Sep 29, 2022 07:53 UTC
  • Russia na  China zinataka kuachiliwa fedha za Afghanistan zilizozuiwa

Wawakilishi wa Russia na China wametaka kuachiwa huru fedha zote za Afghanistan zilizozuiwa. Wamebainisha hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Marekani ilizuia akiba ya fedha za kigeni ya serikali ya Afghanistan mwezi Agosti mwaka jana baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo Kabul na kuidhibiti nchi nzima.  

Anna Ustinova and Gang Shuang Wawakilishi wa Russia na China katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana usiku wameeleza kuwa, fedha zote za Afghanistan ambazo zimezuiwa zinapasa kuachiwa huru ili nchi hiyo iweze kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazoikabili, iboreshe maisha ya Waafghani na kuijenga upya kiuchumi nchi hiyo.  

Ana Ustinova na Gang Shuang wameongeza kuwa, kwa kuzingatia taarifa ya Benki Kuu ya Afghanistan, Russia na China zinataka akiba ya fedha iliyozuiwa ya serikali ya Afghanistan ipatiwe wananchi wa nchi hiyo kikamilifu ili wananchi hao waweze kunufaika na kutumia ipasavyo kutatua mgogoro wa kibinadamu unaowakabili. 

Nayo Ofisi ya Biashara na Uwekezaji ya Afghanistan imesema kitendo cha kuzuia fedha hizo za Afghanistan kimeathiri vibaya uchumi wa nchi hiyo.

Mwezi Februari mwaka huu, Rais Joe Biden wa Marekani alitia saini amri ya utendaji ambapo aliafiki kugawanywa dola bilioni 7 mali ya Afghanistan eti katika mfuko wa masuala ya kibinadamu na kwa ajili ya kuwalipa fidia familia za waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001; suala ambalo limepingwa na kukosolewa vikali na wananchi wa Afghanistan.

Waafghanistan wapinga fedha zao kugawanywa 

 

Tags