Sep 30, 2022 04:33 UTC
  • Marekani yaiwekea Iran vikwazo vingine vipya licha ya mazungumzo ya kuondoa vikwazo vyake haramu

Wizara ya Fedha ya Marekani imeiwekea Iran vikwazo vipya katikati ya mazungumzo ya nchi hiyo na pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanayolenga kuondoa vikwazo vilivyo kinyume na sheria vya Washington dhidi ya Tehran.

Marekani inahesabiwa kuwa nchi inayoongoza kwa uwekaji vikwazo duniani, ikiwa na rekodi kubwa zaidi ya kutumia kila aina ya vikwazo dhidi ya nchi zingine kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, wizara ya fedha ya Marekani imetangaza katika taarifa kwamba imeyawekea vikwazo makampuni 10 na meli moja kwa kisingizio cha kurahisisha usafirishaji wa mafuta ya Iran.
Saa kadhaa zilizopita, duru za kuaminika zilivitaarifu vyombo vya habari vya Magharibi kuwa, Marekani imeweka vikwazo dhidi ya usafirishaji mafuta ya Iran.
Shirika la habari la Reuters nalo pia limeripoti kuwa wizara ya fedha ya Marekani imeyawekea vikwazo makampuni kadhaa ambayo kwa mujibu wa wizara hiyo, yalihusika katika uuzaji wa bidhaa za petrokemikali na mafuta za Iran zenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola kuelekea Kusini na Mashariki ya Asia.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya fedha ya Marekani, hatua hiyo imewalenga madalali na makampuni makuu ya Iran katika Muungano wa Falme za Kiarabu, Hong Kong na India.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken amedai kuwa Washington imeyawekea vikwazo makampuni mawili yaliyoko nchini China kwa sababu ya kukwepa vikwazo vya uuzaji mafuta na bidhaa za petrokemikali za Iran.
Vikwazo hivyo vipya vya Marekani vimewekwa katika hali ambayo serikali ya Rais Joe Biden inadai kuwa inakusudia kuandaa mazingira yanayohitajika kwa ajili ya kurejea nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kupitia mazungumzo.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa serikali ya Biden wamekiri waziwazi na mara kadhaa kwamba, sera ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran imegonga mwamba na kwamba wanakusudia kuirejesha Marekani kwenye JCPOA; lakini hadi sasa, wamekataa kuchukua hatua zinazohitajika ili kurejea kwenye makubaliano hayo.../

 

Tags