Sep 30, 2022 07:22 UTC
  • Korea Kaskazini yajiwekea rekodi ya kufyatua makombora ya balestiki mara tatu ndani ya wiki moja

Korea Kaskazini imefyatua kombora la balestiki kwa mara ya tatu ndani ya wiki moja mara baada ya kumalizika ziara ya makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris nchini Korea Kusini.

Korea Kaskazini, ambayo kila mara inaituhumu Marekani na washirika wake wa kikanda kwamba wanafanya vitendo vya uchochezi na vya kuzusha mivutano katika Peninsula ya Korea, ilikuwa tayari imerusha makombora matatu ya masafa mafupi ya balestiki kuanzia Jumapili asubuhi hadi Jumatano. Ufyatuaji wa makombora hayo ulienda sambamba na mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini na safari ya Harris katika eneo hilo.
Shirika la habari la Yonhap liliripoti jana likiinukuu kamandi ya vikosi vya majeshi ya Korea Kusini, kwamba Korea Kaskazini imefyatua kombora jengine la balestiki.
Kombora hilo ambalo halijatolewa maelezo kamili limerushwa kuelekea Bahari ya Mashariki (Bahari ya Japan).
Kamala Harris akiwa kwenye eneo la mpaka wa pamoja wa Korea mbili

Jeshi la Korea Kusini limetoa taarifa ambayo mbali na kuripoti habari hiyo imefafanua kuwa kombora la balestiki la Korea Kaskazini lilirushwa saa chache baada ya kumalizika ziara ya Kamala Harris, makamu wa rais wa Marekani, na katika siku ya mwisho ya mazoezi ya pamoja ya majini ya Seoul na Washington.

Marekani ilikuwa imetuma Korea Kusini ili kushiriki kwenye luteka hiyo, manowari yake ya kubebea ndege ya USS Ronald Reagan iliyoko pwani ya Japan. 
Harris, ambaye aliwasili Seoul jana asubuhi, alikutana na kuzungumza na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-Yeol na kutembelea pia eneo lisilo la kijeshi linalotenganisha Korea mbili.
Hadi sasa Korea Kaskazini imeshafanya majaribio sita ya nyuklia; na kwa mtazamo wa washirika wa kikanda wa Washington si baidi Pyongyang ikafanya jaribio jengine la saba la nyuklia katika muda mfupi ujao.../

 

Tags