Oct 01, 2022 04:07 UTC

Serikali ya Russia imetoa ushahidi mpya ambao unaonesha jinsi Marekani ilivyohusika katika mripuko wa mabomba ya gesi ya Nord Stream 1 na 2 ambayo yanapeleka gesi ya Russia kwa nchi za Ulaya.

Kuvuja gesi kutoka kwenye mabomba mawili ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 katika Bahari ya Baltic kumezusha mzozo mpya katika uhusiano wa Russia na Marekani na nchi za Ulaya Magharibi.

Shirika la Usalama wa Shirikisho la Russia limetangaza kuwa, Moscow imepata ushahidi madhubuti wa kuthibitisha kuwa, helikopta za Marekani zilipaa kwenye eneo hilo muda mchache kabla ya kutokea mripuko huo. Kiujuumla helikopta hizo za Marekani zilipaa kwa muda wa masaa 9 zikipiga doria karibu na lilipotokea tukio hilo.

Maria Zakharova

 

Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Bi Maria Zakharova amesema kuwa, sehemu ilipovuja gesi kwenye mabomba mawili ya Nord Stream 1 na Nord Stream 2 katika Bahari ya Baltic ni eneo ambalo linadhibitiwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani.

Ameongeza kuwa, eneo lilipotokea tukio hilo ni katika maeneo ya kibiashara na kiuchumi ya Denmark na Sweden ambayo yako chini ya udhibiti wa kijasusi na kijeshi wa Marekani. Pia tusisahau kuwa, nchi hizo za Denmark na Sweden ni wanachama wa NATO na eneo hilo limejaa silaha za Marekani.

Naye Msemaji wa Ikulu ya Russia, Dmitry Peskov amesema, wanasiasa wengi wa Ulaya wamekiri kwamba mripuko huo kwenye mabomba yanayopeleka gesi ya Russia kwa nchi za Ulaya, umetokana na uharibifu uliofanywa kwa makusudi.