Oct 01, 2022 12:02 UTC
  • Nicaragua yakata uhusiano na Uholanzi, yamzuia balozi wa Marekani

Nicaragua imetangaza kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Uholanzi, muda mfupi baada ya kumzuia Balozi wa Marekani kuingia nchini humo kutokana na kile ilichokitaja kuwa ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nicaragua imesema, serikali ya Managua ambayo inakabiliwa na uingiliaji wa kila mara na misimamo ya ukoloni mamboleo ya ufalme wa Uholanzi, imeamua kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na serikali ya Udachi.

Rais Daniel Ortega wa Nicaragua amegusia suala hilo na kusema, "Wale wanaokuja kuwavunjia heshima watu wetu na ardhi yetu, hawapaswi kuruhusiwa tena kuja hapa nchini, na hatutaki kuwa na uhusiano na wale wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi hii."

Huku akizungumza kwa ghadhabu, Rais Daniel Ortega amesema, "Balozi huyo alikuja kuzungumza na Wanicaragua kana kwamba Nicaragua ni koloni la Uholanzi."

Rais Ortega alikuwa anamrejelea Christine Pirenne, Balozi wa Uholanzi kwa nchi hiyo ya Amerika ya Kati, ambaye ofisi yake ipo katika nchi jirani ya Costa Rica.

Rais wa Nicaragua na mkewe

Ikumbukwe kuwa, Uholanzi ilifunga ubalozi wake mjini Managua mwaka 2013, na inaendeshea shughuli zake zote za kidiplomasia katika nchi jirani ya Costa Rica.

Jana Ijumaa, Mke wa Ortega na Makamu wa Rais wa Nicaragua, Rosario Murillo alisema: Balozi mpya wa Washington mjini Managua, Hugo Rodriguez, hatoruhusiwa kuingia katika ardhi ya Nicaragua.

Tags