Oct 02, 2022 02:15 UTC
  • Zakharova: Katibu Mkuu wa UN amevuka mipaka ya mamlaka yake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametangaza kuwa kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba "matokeo ya kura ya maoni ya maeneo mapya hayatakuwa halali na ya kisheria" imevuka mipaka ya mamlaka yake.

Maria Zakharova ameashiria kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuhusu suala la kujiunga maeneo mapya na Russia na akasema: Mashambulizi ya moja kwa moja ya Guterres dhidi ya haki ya kimsingi ya watu wa mikoa ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhia huko mUkraine ya kujiamulia mambo yao ni mfano mwingine wa unafiki na misimamo ya kindumakuwili.

Zakharova ameongeza kuwa, ni jambo lisilokubalika kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa chombo cha propaganda na mashinikizo dhidi ya nchi wanachama, wakati anapaswa kuwa mwakilishi wa wanachama wote kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Matamshi ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia yanafuatia kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio  Guterres aliyesema Alhamisi iliyopita katika taarifa yake kuhusu kura ya maoni iliyofanyika katika mikoa ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhia kwamba uamuzi wowote wa kujiunga maeneo hayo na Russia hautakuwa na tija na unapaswa kulaaniwa.

Antonio  Guterres

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Russia vimechapisha matokeo ya kura za maoni katika mikoa ya Luhansk, Donetsk, Kherson na Zaporizhia na kutangaza kwamba, katika mikoa yote hiyo zaidi ya asilimia 95 ya watu wanataka kujiunga na Russia na kujitenga na Ukraine.