Oct 02, 2022 07:30 UTC
  • Maelfu waandamana Uingereza kulalamikia gharama za juu za maisha

Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya Uingereza, kulalamikia mgogoro wa mfumko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

Maandamano hayo yaliyopangwa na miungano ya wafanyakazi kama vile Umoja wa Uchukuzi na Usafiri wa Baharini RMT, Muungano wa Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na wafanyakazi wa Posta ambao hivi sasa wapo katika mgomo; yameshuhudiwa katika miji yote mikubwa ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu London.

Mmoja wa waandamanaji aliyejitambulisha kwa jina la Tim amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa: Nchi hii imekuwapo katika mgogoro wa kiuchumi kwa muda mrefu sana. 

Amesema wananchi wa Uingereza wameishi katika umaskini na uchochole kwa kipindi kirefu, na hivi sasa mgogoro wa nishati umefanya maisha yawe magumu zaidi kwao.

Mwingine amesema, "kodi ya nyumba ya mmoja wa wafanyakazi wenzangu iliongezwa kwa asilimia 17 wiki iliyopita, katika hali ambayo hatupewi nyongeza ya mishahara kwa kiwango hicho. Nashukuru watu wameamua kusimama, hatuwezi kuendelea kuishi namna hii."

Mtitigo wa uchumi nchini Uingereza

Waandamanaji hao wameitaka serikali kuwapa nyongeza ya mishahara inayoendana na mfumko wa bei za bidhaa wa hivi sasa, ambao haujawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita nchini humo.

Helen, mmoja wa waandamanaji, amekosoa bajeti ya ziada iliyotangazwa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Liz Truss, akisisitiza kuwa, kuwapunguzia kodi watu wanaopata mishahara zaidi ya yuro 150,000 ni hatari kwa taifa, na huo ni mkakati wa kuwanufaisaha matajiri, huku maskini waliowengi wakiendelea kuteseka.

Tags