Oct 02, 2022 12:03 UTC
  • Wabrazili wanapiga kura kuchagua rais mpya, kura za maoni zinaonyesha da Silva atamshinda Bolsonaro katika duru ya kwanza

Takriban wapiga kura milioni 165 wa Brazil wamepiga kura leo, Jumapili, katika uchaguzi wa rais, wakati kura za maoni zinaonyesha kuwa kiongozi wa mrengo wa kushoto wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, anaongoza kwa kishindo dhidi ya rais anayeondoka wa mrengo wa kulia, Jair Bolsonaro, na kuna uwezekano akapata ushindi wa wazi katika raundi ya kwanza.

Kura mbili za maoni zilizochapishwa mapema leo zilionyesha kuwa Lula ana wingi wa kura halali na anaweza kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza, suala ambalo litaepusha uchaguzi mgumu wa marudio mnamo Oktoba 30.

Ikiwa hakuna mgombea yeyote kati ya 11 atapokayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, wagombea wawili ambao watapata kura nyingi watashiriki duru ya pili ya uchaguzi.

Kabla ya uchaguzi wa leo, Lula na Bolsonaro walirushiana tuhuma za ufisadi katika mjadala wao wa mwisho, huku Rais Bolsonaro akimtaja mpinzani wake wa mrengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, kuwa ni mkuu wa genge la wahalifu lililoendesha "serikali ya wezi" kati ya mwaka 2003-2010.

Kwa upande wake, Lula alimtaja Bolsonaro kuwa ni kidhabi "asiye aibu" ambaye serikali yake ilificha ufisadi katika ununuzi wa chanjo wakati wa janga la "Covid-19", ambalo liligharimu maisha ya zaidi ya Wabrazili 680,000.

Luiz Inacio Lula da Silva

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Brazil imealika idadi isiyokuwa ya kawaida ya waangalizi wa kimataifa kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu ya mashambulizi ya Bolsonaro dhidi ya mfumo wa upigaji kura na uwezekano wa kutokea kwa migogoro.

Inafaa kukumbuka kuwa uchaguzi wa leo utaamua ikiwa rais wa zamani ambaye alikuwa gerezani kwa tuhuma za ufisadi au mtu wa mrengo wa kulia ambaye ameshambulia mfumo wa kupiga kura wa nchi hiyo na kutishia kupinga matokeo ya uchaguzi, atarejea madarakani au la.

Rais huyo wa sasa wa Brazil aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema "Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayeweza kumuondoa madarakani", suala ambalo limezusha wasiwasi kwamba yumkini akapinga matokeo ya uchaguzi na kung'ang'ania madaraka.

Jair Bolsonaro

Suala hilo linawafanya wachambuzi wa masuala ya Brazil kuamini kuwa mgombea huyo wa chama cha Liberal anaweza kuiga mfano wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alipokataa kukiri kushindwa katika uchaguzi wa rais wa 2020.

Msimamo huo wa Trump uliwafanya wafuasi wake wavamie Congress mnamo Januari 6, 2021, katika juhudi za kuwazuia wanachama wake kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyoonesha ushindi wa Rais wa sasa Joe Biden. Watu kadhaa waliuawa katika hujuma hiyo ya wafusi wa Trump dhidi ya jengo la Congress. Tukio hilo lilitambuliwa kuwa hatari zaidi kwa Demokrasia ya Marekani.