Oct 03, 2022 02:28 UTC
  • Henry Kissinger
    Henry Kissinger

Henry Kissinger, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, amezitaja juhudi za Washington za kutaka kuiunganisha Ukraine na NATO baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti kuwa ni za kipumbavu.

Henry Kissinger amesema katika Baraza la Washauri la Marekani la Baraza la Mahusiano ya Kigeni kwamba Washington ilijaribu kuwachukua wanachama wote wa zamani wa Umoja wa Kisovieti chini ya mwamvuli wake baada ya kuvunjwa Ukuta wa Berlin.

Kwa mujibu wa Kissinger, "Kwa mtazamo wa Russia, Marekani ilijaribu kuliunganisha eneo lote la (Soviet ya zamani) katika mfumo wa kimkakati chini ya uongozi wa Washington."

Mwanadiplomasia huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 99 ameongeza kuwa: Hali hiyo kimsingi imeharibu ukanda wa usalama wa kihistoria wa Russia; Kwa hiyo, kujaribu kuivuta Ukraine katika shirika la NATO haikuwa sera ya busara ya Marekani.

Kissinger ameendelea akidai kuwa, hajui iwapo amani na rais wa Russia inawezekana, lakini amesisitiza kuwa, nchi za Magharibi zinapaswa kutafuta fursa ya mpango utakaoihakikishia uhuru nchi ya Ukraine na kuiweka katika mfumo wa Ulaya.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani amesema kwamba, nchi za Magharibi na Russia zinapaswa kuingia katika mazungumzo na kuongeza: "Katika mazingira ya sasa ya nyuklia, mazungumzo yanaweza kuwa bora zaidi kuliko "maamuzi ya uwanja wa vita".

Awali Henry Kissinger pia alionya kwamba Marekani "iko ukingoni kuingia kwenye vita na Russia na Uchina juu ya maswala ambayo tunayaibua sisi wenyewe."