Oct 03, 2022 02:31 UTC
  • Kujiunga na Russia majimbo manne ya Ukraine, nembo nyingine ya kufeli Magharibi

Siku ya Ijumaa ya tarehe 30 Septemba 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia alitia saini hati ya kujiunga na Russia majimbo manne ya Ukraine katika sherehe zilizohudhuriwa na wakuu wa majimbo hayo.

Katika sherehe hizo, Putin alisema kuwa, wananchi wa majimbo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporozhye wamefanya maamuzi ya wazi na ya kidemokrasia ya kuamua kujiunga na ardhi ya Russia na kwamba Ukraine ina wajibu wa kuheshimu maamuzi ya wananchi hao. Ni kwa kuheshimiwa matakwa ya wananchi hao tu ndipo amani na usalama utapatikana.

Rais Vladimir Putin pia alisema: Tunautaka utawala wa Kyiv uache vita mara moja na uje kwenye meza ya mazungumzo. Russia iko tayari kufanya mazungumzo na Ukraine. Lakini katika upande wa pili, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amesema: Kyiv kamwe haiwezi kufanya mazungumzo na Russia maadamu Vladimir Putin bado ni rais wa nchi hiyo.

Rais Vladimir Putin wa Russia

 

Kujiunga rasmi na Russia majimbo hayo manne ni tukio muhimu sana katika vita vinavyoendelea huko Ukraine, ambavyo sasa vimeshaingia kwenye mwezi wake wa nane. Ijapokuwa mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Russia illitambua rasmi uamuzi wa kujitenga majimbo mawili ya Donetsk na Luhansk na iliamua kuanzisha operesheni maalumu ya kijeshi ya kuwahami wananchi wa majimbo hayo, lakini kuendelea vita kumebadilisha malengo na shabaha zilizotangazwa hapo awali na Moscow. Warussia walianzisha mashambulio yao katika maeneo ya kusini mashariki, mashariki na kaskazini mwa Ukraine. Lakini baada ya kushindwa medani ya kaskazini, waliamua kuelekeza zaidi nguvu zao kwenye maeneo mawili ya mashariki na kusini mashariki mwa Ukraine na kuteka mikoa minne ya eneo hilo. Baadaye likaja suala la kuitishwa kura ya maoni kwenye majimbo hayo manne ya kuamua kujiunga na ardhi ya Russia au kubakia ndani ya Ukraine ambapo wananchi wa majimbo hayo manne wameamua kurudi katika ardhi mama ya Russia. 

Amma nukta muhimu zaidi katika vita vya Ukraine, ni kufeli nchi za Magharibi hasa Marekani kuizuia Russia kufanikisha malengo yake ya kuingia vitani huko Ukraine. Hadi hivi sasa Wamagharibi wameshatumia zaidi ya dola bilioni 25 kwa ajili ya kuirundikia silaha Ukraine. Silaha hizo ni za mashambulizi ya ardhini na angani. Ni makombora, mizinga, magari ya deraya, droni na kila aina ya silaha waliyoweza kumpa Volodymyr Zelenskyy wamempa, lakini wameshindwa. Tamaa ya Marekani na jeshi la nchi za Magharibi NATO ni kwamba serikali ya Ukraine ingeliweza kuleta mabadiliko katika vita na kuilazimisha Moscow kurudi nyuma na kuachana na malengo yake. Lakini Russia ilijikita zaidi katika kukamilisha udhibiti wake wa majimbo hayo manne; malengo ambayo inaonekana wazi kuwa ndilo hasa lengo la Russia la kuingia vitani huko Ukraine. Serikali ya Moscow imefanikisha malengo hayo huku Marekani na NATO zikishindwa kufanya chochote.

Majimbo manne muhimu sana ya Ukraine yaliyojiunga na Russia, yametoa pigo kubwa kwa serikali ya Kyiv na madola ya Magharibi

 

Majibu yaliyotolewa na Wamagharibi kuhusu kujiunga na Russia majimbo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporozhye pia ni jambo la kuliwekea alama nzito ya swali. Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, amesema, hawawezi kutambua rasmi kujitenga majimbo hayo manne lakini wakati huo huo amesema, NATO haitoingia vitani moja kwa moja bali itaendelea tu kuipa silaha serikali ya Ukraine. Matamshi hayo ameyatoa katika hali ambayo kabla ya majimbo hayo manne kujiunga na Russia, muda wote katibu mkuu huyo wa NATO alikuwa anatoa vitisho vikali dhidi ya Russia. Sasa hivi lakini anasema, NATO haitoingia vitani moja kwa moja ni na Russia. Matamshi hayo ya Stoltenberg yamezidi kuikatisha tamaa serikali inayopenda Umagharibi ya Ukraine ambayo ilikuwa na tamaa kubwa kwamba NATO itaanzisha vita vita vya moja kwa moja vya kupambana na Russia. Si hayo tu, lakini pia viongozi wa Marekani pamoja na kwamba wamepinga uamuzi wa wananchi wa majimbo hayo manne kujiunga na ardhi ya Russia lakini wameishia tu kusema wataendelea kuipa silaha Ukraine, silaha ambazo kama tulivyoona hadi hivi sasa, si zile za kuweza kubadilisha mwenendo wa vita na wala si za kuilazimisha Moscow ilegeze misimamo yake. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, aliyepata hasara zaidi katika mchezo huu wa kisiasa na kivita, ni Ukraine yenyewe. 

Sasa hivi serikali ya Ukraine iko kwenye hali ngumu. Kwanza ni kwamba kuendelea kushambulia majimbo manne ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporozhye maana yake ni kukaribisha majibu makali kutoka kwa Moscow kwani ni sawa na kushambulia ardhi ya Russia. Vile vile serikali ya Ukraine haiwezi kusimamisha vita kutokana na mashinikizo ya nchi za Magharibi hasa Marekani. Viongozi wa NATO nao wametangaza wazi kuwa hawatoingia vitani moja kwa moja kupambana na Russia. Lililobakia ni uhakika mchungu kwamba nchi za Magharibi zimeigeuza Ukraine kuwa sehemu ya kujaribishia silaha zao. Kwa maneno machache ni kwamba nchi za Magharibi hazina mwamana hata chembe. Vita navyo vinaendelea kuigharimu vibaya Ukraine kwa kutaraji kuwa nchi kama Marekani na za Ulaya zitajitolea kikwelikweli kuilinda wakati historia imejirudia kwamba nchi hizo za Magharibi si za kuaminika hata chembe.