Oct 03, 2022 10:54 UTC
  • IEA: Ulaya inakabiliwa na hatari isiyo ya kawaida ya uhaba wa gesi katika msimu ujao wa baridi kali

Shirika la Kimataifa la Nishati IEA limetangaza kwamba kufuatia uamuzi wa Russia wa kusitisha mauzo yake mengi ya gesi kwa Ulaya, bara hilo litakabiliwa na "hatari kubwa isiyo na kifani" ya uhaba wa gesi asilia katika msimu ujao wa baridi kali.

Shirika hilo lenye makao makuu yake mjini Paris Ufaransa, limetangaza katika ripoti yake ya robo mwaka iliyochapishwa leo Jumatatu, kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapaswa kupunguza matumizi yao ya gesi kwa asilimia 13 katika msimu ujao wa baridi kali, ikiwa mauzo ya gesi ya Russia yatakatwa kabisa kufuatia vita vya Ukraine.

Siku ya Ijumaa Umoja wa Ulaya ulikubali kupunguza matumizi ya umeme kwa angalau asilimia tano wakati wa saa za kilele za matumizi hayo.

Ni kiasi kidogo tu cha gesi ya Russia ambacho bado kinaingia kwenye mabomba ya gesi kupitia Ukrainia hadi Slovakia na kuvuka Bahari Nyeusi kupitia Uturuki hadi Bulgaria. Njia nyingine mbili za kusambaza gesi kutoka Bahari ya Baltic hadi Ujerumani kupitia Belarusi na Poland zimekatwa.

Nchi za Ulaya zakabiliwa na hatari ya upungufu wa nishati

Umoja wa Ulaya umejaza asilimia 88 ya hifadhi yake ya gesi, wakati kulingana na tathmini ya Shirika la Kimataifa la Nishati, asilimia 90 ya hifadhi ya gesi ya Umoja wa Ulaya inapaswa kuwa imekamilika iwapo Russia itaamua kukata kabisa gesi yake kuelekea umoja huo.

Biashara nyingi barani Ulaya zimepunguza matumizi yao ya gesi asilia na hata viwanda vinavyotumia nishati kubwa katika uzalishaji wa bidhaa zao kama vile uzalishaji wa chuma na mbolea vimesimamisha kabisa shughuli zao.

Lengo la hatua hiyo ni kuzuia kupungua kwa akiba ya gesi kwa kiwango ambacho kitailazimu serikali kutoa gesi kwa mgao kwa maeneo ya biashara.

Licha ya Marekani na washirika wake kuiwekea Russia vikwazo lakini bado nchi hizo za Magharibi zinahofia kwamba kushadidi vikwazo dhidi ya nchi hiyo katika sekta za kiuchumi, hususan sekta ya mafuta na gesi, huenda kukavuruga zaidi hali ya kiuchumi ya Ulaya na  masoko ya nishati duniani.

Tags