Oct 04, 2022 12:12 UTC
  • Baraza la Shirikisho la Russia lapitisha mpango wa kuyaunganisha maeneo 4 ya Ukraine na nchi hiyo

Baraza la Shirikisho la Russia leo limeidhinisha mikataba ya kuzikubali Jamhuri ya Watu wa Donetsk na Jamhuri ya Watu wa Luhansk pamoja na maeneo ya Kherson na Zaporizhia kuwa sehemu ya ardhi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, mpango wa kuyaunganisha maeneo manne ya Ukraine na Russia umepitishwa kwenye baraza hilo la shirikisho wakati bunge la Duma la nchi hiyo liliidhinisha hapo jana mikataba inayohusiana na suala hilo.
Kura ya maoni ya kutaka kujiunga na Russia maeneo manne ya mkoa wa Donbas ulioko mashariki mwa Ukraine ilifanyika kuanzia Septemba 23 hadi 27.
Kulingana na matokeo rasmi, 99.23% ya wapiga kura katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk, 98.42% katika Jamhuri ya Watu wa Luhansk, 93.11% katika mkoa wa Zaporizhia na 87.05% ya wakazi wa mkoa wa Kherson wametaka kuwa sehemu ya Shirikisho la Russia.
Rais Vladimir Putin

Baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni, Rais Vladimir Putin wa Russia na viongozi wa jamhuri za Donetsk na Luhansk pamoja na viongozi wanaounga mkono Russia katika mikoa ya Zaporizhia na Kherson walitia saini mikataba ya makubaliano ya kuyakubali maeneo hayo kuwa sehemu ya Russia.

Katika jibu lao kwa hatua hiyo, marais wa nchi tisa wanachama wa shirika la kijeshi la NATO katika Ulaya ya Kati na Mashariki walitangaza siku ya Jumapili kuwa hawatatambua kamwe kuunganishwa na Russia maeneo hayo manne ya Ukraine.
Taarifa ya uamuzi wa kupinga hatua hiyo ilitiwa saini na marais wa Romania, Jamhuri ya Czech, Estonia, Latvia, Lithuania, Macedonia Kaskazini, Montenegro, Poland na Slovakia.../