Oct 05, 2022 02:12 UTC
  • Kampeni za mabinti wa Kiislamu Ufaransa za kupigania vazi la hijabu mashuleni

Licha ya kuweko aina kwa aina ya sheria na mibinyo ya kuzuia vazi la hijabu kwa mabinti na wanawake wa Kiislamu nchini Ufaransa, lakini wasichana wanaovaa hijabu katika nchi hiyo ya bara Ulaya wanatafuta njia za kutatuliwa tatizo hilo wakitumia mbinu nas mikakati mbalimbali.

Wasichana hao wanaovaa vazi la staha ya mwanamke wa Kiislamu hijabu nchini Ufaransa wamezidisha kampeni ya kuwahamasisha wenzao kuvaa vazi hilo la Kiislamu wakitumia mitandao ya kijamii. Mabanati hao wanawahimiza wasichana wengine kuvaa mavazi ya stara ya kidini na hata kutekeleza ibada ya Swala kwa siri katika taasisi za elimu kwa kuweka machapisho kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok.

Waislamu walio wachache nchini Ufaransa daima wamekuwa wakikabiliwa na matatizo tofauti hasa katika suala la vazi la hijabu na vikwazo kwa wanawake wenye kuvaa vazi hilo la stara kwa kuzingatia sheria za kilaiki zinazotawala nchi hiyo.

Mwaka 2011, Ufaransa ilipiga marufuku vazi la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, kwa kupitisha sheria iliyokosolewa na watetezi wa haki za binadamu, na baada ya hapo, nchi zingine za Ulaya kama Denmark, Austria, Uholanzi na Bulgaria zilifuata mkondo na kupitisha sheria kama hizo.

 

Serikali ya Ufaransa pia imewasilisha sheria inayokataza kuwepo kwa dini katika shule za nchi hiyo, jambo ambalo limezidisha mivutano ya kidini nchini humo.

Kwa kuzingatia hali hiyo wasichana wadogo wa Kifaransa waliovalia hijabu wanatumia mtandao wa kijamii wa Tik Tok kujaribu kutatua matatizo yanayohusiana na marufuku ya kuvaa mavazi ya Kiislamu mashuleni, na kuhimiza zaidi kupuuzwa sheria ya 2004 ya kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule za Ufaransa.

Wanaume pia wameunga mkono hatua hiyo ya mabanati wa Kiislamu nchini Ufaransa na hata kuchukua hatua za kuwahamasisha waendelee na kampeni hiyo. Hata hivyo hatua hiyo ya mabinti wa Kiislamu imekabiliwa na majibu mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Ufaransa.

Miongoni mwao ni Waziri wa Elimu wa Ufaransa, Pap Ndiaye ambaye alitangaza Jumamosi iliyopita kwamba, ripoti za ukiukwaji wa sheria ya 2004 inayokataza vazi la hijabu zimeongezeka tangu mwanzo wa mwaka wa masomo katika shule za Ufaransa. Kadhalika amesema kuwa, katika miezi sita ya awali ya mwaka huu kumeripotiwa matukio 241 ya ukiukaji wa sheria hii na kuongeza kuwa, ukiukwaji mwingi wa sheria hiyo unasababishwa na kuvaa nguo kama vile abaya au baibui ambako kunaonekana kuongezeka.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya IFOP unaonesha kuwa, asilimia 57 ya walimu walio na chini ya umri wa miaka 30 wanaunga mkono vazi la hijabu miongoni mwa wanafunzi katika shule za Ufaransa.

Waandamanaji wakiwa na beramu lenye ujumbe: Hijabu ni utambulisho wa mwanamke wa Kiislamu

 

Itakkumbukwa kuwa, Agosti mwaka huu (2022), Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza mjini Geneva Uswisi kwamba, hatua ya Ufaransa ya kupiga marufuku mwanamke kuvaa hijabu katika kozi ya masomo kwa watu wakubwa iliyokuwa ikifanyika katika sekondari moja, ilikiuka wazi mkataba wa kimataifa unaohusiana na haki za kiraia na kisiasa. Ukweli wa mambo ni kuwa, msimamo wa Umoja wa Mataifa kwamba, wanawake wa Kiislamu wana haki ya kuvaa hijabu nchini Ufaransa kwa hakika ulikuwa ni kupiga muhuri wa kubatilisha  madai ya viongozi wa Paris ya kuweko uhuru na haki kwa raia wan chi hiyo ya bara Ulaya.

Ni kwa muda mrefu sasa ambapo mabinti na wanawake wa Kiislamu nchini Ufaransa wamekuwa wakiandamwa na mashinikizo ya kila aina, mibinyo na ukandamizaji kutokana tu na kuvaa kwao vazi la stara ya mwanamke wa Kiislamu hijabu. Moja ya vizingiti wanavyokabiliwa navyo ni kunyimwa fursa ya kusoma katika nchi hiyo ambayo ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na kushadidi mashinikizo dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa ni mambo ambayo yamechukua wigo mpana katika nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

Katika kipindi cha uongozi wa Rais Emmanuel Macron maisha ya Waislamu nchini humo yamekuwa magumu zaidi kwani mbali na kukabiliwa na mibinyo, kumepasishwa sheria mbalimbali dhidi ya Waislamu na vituo vya Kiislamu. Utendaji wa Macron pamoja na hatua zake anazochukua dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa ni katika kutekeleza misingi ya usekulari ambayo inataka kuweko mapambano amilifu dhidi ya dini na nembo zake katika jamii.

Chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni

 

Kimsingi ni kuwa, Macron hana mtazamo chanya kabisa na Uislamu na ndio maana amekuwa akiunga mkono kila hatua yenye chuki dhidi ya Uislamu, inayolenga kudhoofisha dini hii au hata inayomvunjia heshima Mtume Muhammad (saww).

Mifano ya wazi ni hatua yake ya kutetea vibonzo na vikatuni vya gazeti la Charlie Hebdo vilivyokuwa vikimvunjia heshima Mtume, kufukuzwa Waislamu, kufungwa misikiti na vituo vya Kiislamu sambamba na kuwasilisha muswada wenye lengo la kuimarisha mfumo wa kisekulari ingawa lengo lake hasa la muswada huo ni kudhoofisha Uislamu katika jamii ya Ufaransa. Sambamba na hayo, katika kipindi cha uongozi wake, mashinikizo dhidi ya wanawake na mabinti wa Kiislamu ya kuwazuia wasivae hijabu yamechukua mkondo na wigo mpana zaidi ikilinganishwa na huko nyuma.

Masoud Shajareh Mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu anasema: "Macron anauhujumu Uislamu moja kwa moja na anasema Uislamu uko kwenye mgogoro, katika hali ambayo ukweli ni kuwa mgogoro halisi uko katika sera za Ufaransa na misimamo ya viongozi wa Ulaya."

Tags