Oct 05, 2022 07:10 UTC
  • Kashfa ya ngono yatikisa Ligi ya Soka ya Wanawake ya Marekani na Shirikisho la Soka la nchi hiyo

Katika ripoti yake, Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani amefichua kashfa ya ngono katika Ligi ya Soka ya Wanawake ya Marekani na Shirikisho la Soka la nchi hiyo.

Sally Q. Yates, Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Marekani, amesema uchunguzi unaonyesha kuwa makocha wa timu za soka wamefanya unyanyasaji wa kisaikolojia na kingono dhidi ya wanasoka wa kike na shirikisho la soka la nchi hiyo.

Sally Yates amesema, unyanyasaji wa kingono, kisaikolojia na mienendo miovu katika Ligi ya Soka ya Wanawake ya Marekani haukuhusu timu moja, kocha mmoja au mchezaji mmoja, na kwamba uhalifu huo umefanyika kwenye timu kadhaa; na  makocha kadhaa wamefanya unyanyasaji wa kisaikolojia na kingono dhidi ya wanawake wachezaji wa soka.

Kashfa hiyo ya manyanyaso ya kingono dhidi ya wachezaji wa kike wa mpira wa miguu nchini Marekani iliibuka baada ya wachezaji wa zamani wa NWSL, Sinead Farrelly na Mana Shim kujitokeza hadharani na madai ya kunyanyaswa na kulazimishwa kufanya ngono na kocha wa zamani wa timu ya North Carolina Courage, Paul Riley. Kocha huyo alitumuliwa baada ya kufichuliwa kashfa hiyo. 

Uchunguzi ulibaini kuwa, tatizo la unyanyasaji wa kingono wa wanasoka wa kike nchini Marekani ni kubwa sana. Makocha wakuu watano kati ya 10 wa Ligi ya Soka ya Wanawake ya Marekani (NWSL) msimu uliopita aidha walifutwa kazi au kujiuzulu kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.

Rais wa Soka wa Marekani, Cindy Parlow Cone ameyata matokeo ya uchunguzi huo kuwa ni "ya kuhuzunisha na ya kutia wasiwasi sana."

Tags