Oct 05, 2022 07:12 UTC
  • Mauaji ya Hazara wa Afghanistan na sera za kindumakuwili za nchi Magharibi

Idadi kubwa ya wanawake na wasichana wa Afghanistan wamefanya maandamano katika eneo la Dashte Barchi magharibi mwa Kabul, wakidai haki zao na kukomeshwa kwa mashambulizi ya kigaidi dhidi ya kaumu ya Hazara.

Askari wa serikali ya Taliban wamekandamiza maandamano hayo kwa kuwafyatulia risasi na kuwapiga wanaandamanaji. Waandishi kadhaa wa habari pia walitimuliwa kutoka mahali hapo. Maandamano hayo wa watu wa kaumu ya Hazara ambao ni Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Afghanistan, yamefanyika baada ya hujuma ya kigaidi ya Ijumaa iliyopita iliyolenga kituo cha elimu na kuua zaidi ya wanafunzi 50 waliokuwa wanashiriki mtihani wa kuingia chuo kikuu. Makumi wa wanafunzi wengine wa kike pia walijeruhiwa. 

Nukta muhimu ya kuzingatiwa hapa ni kwamba wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, hasa haki za wanawake, wamekaa kimya dhidi ya uhalifu huo wa kutisha, ambao waathirika wake wengi ni wasichana waliokuwa wakishiriki mtihani kwenye taasisi ya elimu. Hata hivyo tabia hii ya Marekani na washirika wake ambao wamefanya uhalifu na jinai za kutisha nchini Afghanistan kwa zaidi ya miaka ishirini, ni jambo la kawaida. Sayyid Isa Hosseini, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: "Kutenda uhalifu na ugaidi ni mambo ya kawaida kwa Marekani na washirika wake. Haishangazi kuona Marekani na washirika wake wakikaa kimya mbele ya jinai ya Ijumaa iliyopita eneo la Dashte Barchi kwa kutilia maanani kwamba mauaji ya wanafunzi wa kike wakati wa mtihani yalifanywa na mawakala wa Marekani."

Ukweli ni kwamba kimya cha Marekani kuhusu ukiukwaji wa haki za wanawake hakishuhudiwi tu nchini Afghanistan, bali pia msimamo huo wa kinafiki unaweza kuonekana katika maeneo mengine ya dunia, kama vile kuhusiana na magendo ya wanawake na wasichana kutoka Ukraine hadi nchi za Ulaya na kupufumbiwa macho uhalifu na ubakaji wa wanawake wa Marekani kwenyewe. Takwimu zinaonesha kuwa, faida inayotokana na unyonyaji wa kuwatumia wanawake katika biashara haramu ya ngono inafikia euro bilioni 7 kwa mwaka, na fedha zinazopatikana kutokana na magendo ya mamia ya maelfu ya wanawake na wasichana wanaosafirishwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwa ni pamoja na Ukraine, huingia kwenye mifuko ya mabepari wa Magharibi. 

Soroush Amiri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema: "Wanawake katika maeneo mbalimbali ya dunia ni wahanga wa uroho na ulafi wa mabepari wa Magharibi. Faida kubwa inayotokana na unyonyaji wa kingono imekuwa sababu ya kuanzishwa rasmi tasnia ya biashara ya ngono na kuuzwa miili ya wasichana na wanawake, na suala hilo linakadhibisha madai ya nchi za Magharibi eti ya kutetea haki za wanawake." 

Vyovyote iwavyo, maandamano ya wasichana na wanawake wa Afghanistan ya kutaka kuhakikishiwa usalama wao ni kilio cha wanyonge ambao wamekuwa wakiteswa kihistoria na serikali na makundi mbalimbali nchini Afghanistan. Hivyo basi, watu, haswa wanawake wa Afghanistan, wanatarajia kuwa kundi la Taliban ambalo limechukua mamlaka ya nchi hiyo, litawafikisha wahusika wa uhalifu huo kwenye vyombo vya sheria kwa kuchukua hatua zinazohitajika sambamba na kuhakikisha usalama wa raia. Suala hili linapata umuhimu zaidi kwa kutilia maanani juhudi zinazofanywa na maadui wa Afghanistan za kuzusha migawanyiko ya kikabila na kidini nchini humo. 

Ni wazi kwamba, makelele ya vyombo vya habari vya Kimagharibi kuhusu haki za wanawake ni nara tupu zenye malengo ya kisiasa, na vyombo vya habari vya nchi hizo vinafuata sera za kindumauwili sawa kabia na serikali za nchi zao. 

Kwa mfano, uhalifu unaofanyika dhidi ya wanawake nchini Marekani, mashambulizi dhidi ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan na mateso na manyanyayso ya wanawake waliokimbia makazi yao nchini Ukraine, haviakisiwi ipasavyo katika vyombo vya habari, na mara nyingi kufumbiwa macho na mashirika ya habari ya nchi za Magharibi. Kwa upande mwingine, masuala ya wanawake katika nchi zisizofungamana na Magharibi, yamekuwa chombo cha mashinikizo dhidi mifumo ya kisiasa ya nchi hizo zisizokubaliana na sera za kibeberu.

Matukio ya hivi majuzi nchini Iran ni mfano wa sera za undumakuwili wa vyombo vya habari vya Magharibi, sera ambazo sasa zimetambuliwa na walimwengu.

Tags