Oct 05, 2022 13:30 UTC
  • Russia yaionya Marekani kuhusu 'mapigano ya kijeshi ya moja kwa moja' ikiwa silaha zaidi zitatumwa Ukraine

Russia inasema uamuzi wa Marekani wa kusafirisha silaha zaidi hadi Ukraine unaleta "tishio la hivi sasa" kwa maslahi ya Moscow na kuongeza hatari ya makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya Russia na Magharibi.

Hatua ya Marekani na washirika wake ya kusambaza silaha na zana za kijeshi nchini Ukraine haipelekei tu kuongezeka umwagaji damu wa muda mrefu na majeruhi wapya, bali pia inongeza hatari ya mapigano ya moja kwa moja ya kijeshi kati ya Russia na nchi za Magharibi,"  Hayo yamesemwa leo Jumatano na Balozi wa Russia nchini Marekani Anatoly Antonov.

"Tunaona hili kama tishio la hivi sasa kwa maslahi ya kimkakati ya nchi yetu," amesema, baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuahidi mfuko mpya wa msaada wa kijeshi wa dola milioni 625 kwa Ukraine siku ya Jumanne.

Silaha hizo za Marekani zitajumuisha mtambo wa mfumo wa kuvurumisha maroketi ujulikano kama (HIMARS), ambao unaripotiwa kutumika katika mashambulio ya hivi majuzi ya Ukraine dhidi ya vikosi vya Russia, na kusababisha vikosi hivyo kurudi nyuma katika baadhi ya maeneo.

Wiki iliyopita, Washington pia ilizindua kifurushi cha silaha cha dola bilioni 1.1 kwa Ukraine, ambacho kilijumuisha mifumo 18 ya HIMARS, maroketi , aina mbalimbali za mifumo ya kukabiliana na ndege zisizo na rubani na mifumo ya rada.

Rais Biden wa Marekani

Tangu Russia ianzishe oparesheni zake za kijeshi nchni Ukriane mwezi Februari hadi sasa, Marekani imeipa nchi hiyo msaada wa zaidi ya dola bilioni 16.8.

Hayo yanajiri wakati ambao siku ya Ijumaa ya tarehe 30 Septemba 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia alitia saini hati ya kujiunga na Russia majimbo manne ya Ukraine katika sherehe zilizohudhuriwa na wakuu wa majimbo hayo. Katika sherehe hizo, Putin alisema kuwa, wananchi wa majimbo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporozhye wamefanya maamuzi ya wazi na ya kidemokrasia ya kuamua kujiunga na ardhi ya Russia na kwamba Ukraine ina wajibu wa kuheshimu maamuzi ya wananchi hao. Ni kwa kuheshimiwa matakwa ya wananchi hao tu ndipo amani na usalama utapatikana.