Oct 06, 2022 11:36 UTC
  • Polisi wa zamani aua makumi ya watoto wa chekechea Thailand

Watu wasiopungua 34, wengi wao wakiwa watoto, wameuawa mapema leo Alkhamisi nchini Thailand baada ya polisi wa zamani kufyatua risasi kituo cha kulea watoto katika mkoa wa Nong Bua Lamphu.

Gazeti la Bangkok Post limeripoti kwamba Naibu Mkuu wa Polisi wa Kitaifa, Torsak Sokwimul amesema kuwa "watu 34, wakiwemo watoto 22, wamethibitishwa kuuawa, baada ya aliyekuwa polisi, Panya Khamrab, kufyatua risasi ndani ya kituo hicho wilayani Na Klang."

Afisa huyo ameongeza kuwa watu wasiopungua 12 walijeruhiwa katika tukio hilo, 8 kati yao wakiwa katika hali mbaya. Sababu ya tukio hiyo bado haijafahamika.

Polisi wamesema Banya, 34, alifukuzwa kutoka kwenye jeshi la polisi mnamo Juni 15, kwa kupatikana na tembe za kulevya za methamphetamine.

Polisi huyo wa zamani alifanikiwa kutoroka kutoka eneo la tukio, na Ofisi Kuu ya Upelelezi imesema - kwenye ukurasa wake wa Facebook - kwamba polisi huyo wa zamani alijipiga risasi baadaye, baada na kumuua mke na mtoto wake mwenyewe.

Ingawa matukio ya ufyatuaji risasi kwenye maeneo ya umma ni nadra nchini Thailand, lakini 2020 nchi hiyo ilikumbwa na mtikisiko mkubwa wakati mwanajeshi alipoua watu wasiopungua 29 na kujeruhi wengine 57 katika maeneo 4 tofauti.