Oct 07, 2022 02:34 UTC
  • Ufisadi wa kimaadili watikisa makanisa ya Uingereza

Utafiti mpya uliofanywa katika makanisa ya Uingereza unaonyesha kina cha utovu wa maadili wa makasisi na wafanyakazi wa taasisi hizo za kidini.

Katika uchunguzi huo ambao umetajwa na vyombo vya habari vya Uingereza kuwa uchunguzi wa kina zaidi wa kesi za unyanyasaji wa kingono, kumegundulika kesi 383, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa watu wanaoishi katika mazingira magumu na watoto wadogo. Maafisa wa kanisa wanasema kesi hizi zinahitaji uchunguzi na mazingatio makubwa zaidi.

Askofu Mkuu wa Canterbury na York, ambayo inatambuliwa kuwa mamlaka ya juu zaidi ya kidini nchini Uingereza, ameomba msamaha kutokana na matokeo ya uchunguzi huo.

Uchunguzi kama huo uliofanyika miaka kumi na miwili iliyopita pia ulibaini kuwepo kesi kadhaa za ufisadi wa kimaadili katika kanisa la Uingereza. Hata hivyo ripoti iliyotolewa Jumatano wiki hii, imekosoa vikali utamaduni na ufuska ndani ya kanisa hilo.

Ripoti zinasema, kesi 168 kati ya 383 za ufuska zilizotambuliwa, zinahusiana na unyanyasaji wa watoto kingono, na kesi 149 zinahusiana na unyanyasaji wa watu wazima walio katika mazingira magumu.

Wakati huo huo, kulingana na vyombo vya habari vya Uingereza, kuna visa vingi vya ufisadi wa maadili katika kanisa hilo kuliko vile vinavyotangazwa kwenye takwimu rasmi. 

Matokeo ya ripoti hiyo yanaonesha kuwa, viongozi wanaotuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono ni pamoja na makasisi 242, wafanyikazi 53 wa kanisa na 41 wa kujitolea. Watu wengine ama hawana cheo tena kanisani au utambulisho wao haujarekodiwa.

Inatupasa kueleza hapa kuwa, kashfa za utovu wa maadili nchini Uingereza hazihusu makanisa ya nchi hiyo pekee bali taasisi nyingine za serikali pia zimechafuliwa na tatizo hilo. 

Miaka minne iliyopita, ripoti kuhusu ufisadi wa kimaadili katika Bunge la Uingereza ilizusha mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari.

Kulingana na utafiti uliofanywa katika Bunge la Uingereza, ufisadi wa kimaadili na unyanyasaji wa kingono miongoni mwa wawakilishi wa nchi hiyo umekuwa jambo la kawaida kutokana na kunyamaziwa kimya wa maafisa wakuu wa taasisi hiyo ya kisiasa.