Oct 07, 2022 11:30 UTC
  • Russia: Rais wa Ukraine anachochea vita vya tatu vya dunia

Ikulu ya Russia, Kremlin imemshutumu Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine kwa kujaribu kuzusha vita vya tatu vya dunia, baada ya kulitaka shirika la kijeshi la NATO lianzishe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Russia ili kuizuia isitumie silaha za nyuklia.

Akihutubia Taasisi ya Australian Lowy, Zelensky amesema, lazima NATO ihakikishe Moscow haitumii silaha za nyuklia dhidi ya vikosi vya Kiev. Na ili kufanya hivyo, akatoa wito kwa kambi hiyo ya kijeshi inayoongozwa na Marekani na jumuiya ya kimataifa kutangulia kufanya mashambulizi dhidi ya Russia kwa ajili ya kile alichosema "ijue nini cha kutarajia" ikiwa itakuja kuamua kuzitumia silaha za nyuklia.
Katika hotuba yake hiyo aliyotoa kwa njia ya intaneti, Zelensky amesema: "NATO ifanye nini? Ondoa uwezekano wa Russia kutumia silaha za nyuklia. Kwa mara nyingine tena natoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, kama ilivyokuwa kabla ya Februari 24: kutangulia kushambulia, ili wao [Russia] wajue kitakachowapata ikiwa watatumia, na si vinginevyo."
Peskov

Ikulu ya Russia, Kremlin imekemea na kulaani pendekezo hilo ililotolewa na rais wa Ukraine.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema, maoni ya kiongozi huyo wa Ukraine si kitu kingine isipokuwa ni jaribio la kuzusha vita vya dunia, ambavyo vitasababisha "matokeo mabaya yasiyotarajiwa."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia imemshutumu Zelensky kwa kujaribu kuchochea vita vya nyuklia, huku msemaji wake Maria Zakharova akisema kwamba "kila mtu kwenye sayari" anapaswa kutambua kuwa kiongozi kibaraka "asiye na umakini" wa Ukraine, ambaye amemiminiwa silaha chungu nzima, amegeuka “zimwi, ambalo mikono yake inaweza kuiangamiza sayari".../

 

Tags