Oct 07, 2022 11:34 UTC
  • Jeshi la Marekani limeua raia wasiopungua 71,000 nchini Afghanistan

Askari wa jeshi vamizi la Marekani wameua raia wasiopungua elfu 71 wa Afghanistan katika kipindi cha miaka ishirini ya kuikalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.

Mnamo Oktoba 7, 2001, Marekani na washirika wake waliishambulia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha amani na usalama nchini humo.
Baada ya miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu Afghanistan sambamba na kufanya jinai zisizohesabika zikiwemo za kuteketeza miundombinu ya kiuchumi na kiafya, mwishoni mwa mwezi Agosti 2021 wanajeshi wa Marekani hatimaye waliondoka kwa aibu na fedheha katika ardhi ya nchi hiyo; na mnamo katikati ya mwezi huo, kundi la Taliban likarudi tena madarakani huko Afghanistan.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, serikali ya Taliban imetangaza katika taarifa iliyotoa leo kwamba, miaka ishirini na moja iliyopita katika siku kama hii (tarehe 7 Oktoba), Marekani iliishambulia kijeshi Afghanistan bila kibali wala kuwa na sababu za kimantiki, ambapo matokeo ya hujuma hiyo ni kuuawa zaidi ya raia 71,000 wa Afghanistan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zaidi ya askari 78,000 wa jeshi na polisi ya Afghanistan waliuawa pia katika miongo hiyo miwili ya uvamizi.
Askari wa jeshi vamizi la Marekani walipokuwa Afghanistan

Katika taarifa yake hiyo iliyotoa kwa mnasaba wa kutimia miaka 21 tangu Marekani ilipoivamia kijeshi Afghanistan, serikali ya Taliban imeongeza kuwa, mashambulizi ya Marekani na vita vya Afghanistan vimesababisha pia mamilioni ya watu katika nchi hiyo kupoteza makazi yao.

Taarifa ya Taliban imeeleza kuwa, hivi sasa Afghanistan haikaliwi tena na askari wa majeshi vamizi; na raia wake wanaishi kwa uhuru; na kwa mara nyingine tena serikali ya Taliban inatoa hakikisho kuwa Afghanistan si tishio kwa nchi yoyote ile na haitaruhusu ardhi ya nchi hiyo itumike dhidi ya nchi nyingine.
Lakini mkabala na hayo, inazitaka pia nchi zingine zisiwe na msimamo wa kihasama kuhusiana na Afghanistan wala kuweka vizuizi dhidi ya amani, uthabiti na maendeleo ya nchi hiyo.
Ijapokuwa uvamizi wa Marekani na ukaliaji kwa mabavu ardhi ya Afghanistan umehitimishwa, lakini nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi, kijamii, ukosefu wa ajira na umaskini uliokithiri ambavyo vimesababishwa na miongo miwili ya vita, uvamizi na ukaliaji huo wa ardhi kwa mabavu uliofanywa na Marekani dhidi ya nchi hiyo.../

 

Tags