Feb 18, 2017 04:42 UTC
  • Jumamosi, Februari 18, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1438 Hijria mwafaka na tarehe 18 Februari 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 756 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jamadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqiqiin katika mji wa Hillah nchini Iraq. Allamah Hilli alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usuulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul" na "Tahswilul Najat na “al Kafiya”." Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria. ***

Fakhr al-Muhaqiqiin

Katika siku kama ya leo miaka 701 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Mohammad bin Muhammad al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj. Al-Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al-Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al-Madkhal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.***

Abu Abdullah Mohammad bin Muhammad al-Abdari al-Fasi 

Miaka 453 iliyopita katika siku kama ya leo, Michel Angelo Buonarroti mchoraji, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na miaka 89. Michel Angelo alizaliwa mwaka 1475 Miladia na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo. Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kuu za kisanaa zilizofanywa na Michel Angelo katika zama zake hizo. ***

Michel Angelo Buonarroti

Katika siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, vikosi vya mkoloni Mfaransa ambavyo vilikuwa vimeanza kuikalia kwa mabavu nchi ya Algeria tangu mwaka 1830, vilishindwa vibaya na vikosi vya Abdul-Qadir al-Jazairi kiasi kwamba, theluthi moja ya wanajeshi wa Ufaransa waliuawa na nusu ya waliobakia kushikiliwa mateka. Katika hali hiyo, ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa ufaransa kushindwa vibaya namna hiyo barani Afrika ili iwe kukukusanya nguvu tena, Ufaransa iliomba suluhu. Hata hivyo Amir Abdul-Qadir al-Jazairi alilikubali ombi hilo baada ya kupita miaka miwili ambapo takribani ardhi yote ya Algeria ilikuwa imeshakombolewa kutoka katika uvamizi wa mkoloni Mfaransa. ***

Abdul-Qadir al-Jazairi

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 na kupora maliasi za nchi hiyo kwa karibu karne nne. Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia mamlaka ya ndani baada ya kudhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendesha makoloni yake. Hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ilipatia uhuru wake. ***

Bendera ya Taifa ya Gambia

Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, Ayatullah Sayyid Muhammad Swadiq Sadr mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Iraq aliuawa shahidi na magaidi katika mji mtakatifu wa Najaf nchini humo. Wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maandamano mbalimbali kufuatia kuuawa kwa ulamaa huyo mkubwa na kuutaja utawala wa zamani wa Baath huko Iraq kuwa ndio uliomuuwa shahidi Ayatullah Sadr. Utawala wa zamani wa Iraq Baath ulifanya mauaji mengi dhidi ya maulamaa wa kidini katika siasa zake za kuidhoofisha Hauza ya Najaf na wanazuoni wa nchi hiyo, tangu uliposhika hatamu za uongozi huko Iraq mwaka 1968. ***

Ayatullah Sayyid Muhammad Sadiq Sadr

Na miaka 7 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran iliyojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi. Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki. Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa, pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manowari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu duniani na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo.***

Manowari ya Jamaran

 

Tags

Maoni